Wakulima wa Kirinyaga kunufaika na viwanda tisa vya uongezaji ubora bidhaa

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, December 8  2017 at  06:24

Kwa Muhtasari

Kaunti ya Kirinyaga kwa ushirikiano na taasisi ya ustawishaji viwanda (KIE) itajenga vituo tisa vya kusaidia wakulima kuongeza ubora bidhaa zao za kilimo.

 

KAUNTI ya Kirinyaga kwa ushirikiano na taasisi ya ustawishaji viwanda (KIE) itajenga vituo tisa vya kusaidia wakulima kuongeza ubora bidhaa zao za kilimo.

Kwa mujibu wa katibu wa kilimo katika Kaunti hiyo, Stanley Gachugo, viwanda hivyo vitawasaidia wakulima wa eneo hilo kujihakikishia pato bora sokoni kinyume na hali ya sasa ambapo wao huuza bidha zisizoongezewa ubora.

Akiongea katika kikao cha waandishi wa habari ofisini mwake, Gachugo alisema kuwa kwa sasa kuna hitilafu kubwa katika soko ambapo waagizaji kutoka nje hununua mazao ya wakulima kwa bei duni kisha wao kwenda kuongezea ubora hivyo basi kuwafaa wananchi wao na nafasi za kazi.

Aidha, bidhaa hizo huishia kuletwa hapa nchini tena zikiwa na bei ya juu hivyo basi wakulima waliozizalisha wakifanywa kuwa soko tena la faida kwa mataifa hayo.

"Hali hiyo ni kinyume na azima yetu ya kuunda nafasi za kazi na kuhakikisha kuwa wakulima wetu ndio wanaonufaika zaidi na mikakati ya mauzo," akasema.

Alisema kuwa mradi huo utakaogharimu Sh1.2 bilioni utalenga sekta za kilimo cha mboga na matunda, ambao kwa sasa ndio wanaoumia zaidi katika sakata hiyo ya uthibiti wa masoko.

"Wakulima wa nyanya, macadamia, avocado, maembe na ndizi ndio tutafaa kwa mradi huu. Aidha, kuna wakulima ambao wanazalisha asali na hata wao tutawajumuisha katika mradi huu wa awamu ya kwanza," akasema.

Gachugo alisema kuwa mkataba wa maelewano kati ya serikali ya Kaunti na taasisi hiyo ya KIE unatazamiwa kutekelezwa punde tu pesa za matumizi ya bajeti ya mwaka 2017/18 zitaanza kutekelezwa.

"Kabla ya mwaka huu kutamatika, tutakuwa tumemalizana na awamu ya kwanza ya mradi huo na kisha tuzindue awamu nyingine ya kusambaza viwanda hivyo hadi kwa sekta zingine ambazo zinachipuka mashinani," akasema.