http://www.swahilihub.com/image/view/-/4776560/medRes/1204466/-/ujsm8f/-/DNNYERISIASA2605fA%25282%2529.jpg

 

Serikali kuanza kununua mavuno ya mchele kutoka kwa wakulima

Mwangi Kiunjuri

Waziri Mwangi Kiunjuri akihutubu awali. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  14:25

Kwa Muhtasari

Ni hatua sawa na jinsi serikali hununua mahindi kutoka kwa wakulima hapa nchini Kenya.

 

WAZIRI wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri amewaahidi wakulima wa mpunga hapa nchini kuwa serikali itaanza kuwanunulia mavuno yao sawa na vile hununulia wakulima wa mahindi zao hilo.

Amesema kuwa kwa sasa hakuna sera maalum ya ununuzi nafaka hapa nchini lakini atahakikisha hata mchele umeingizwa katika darubini ya serikali ya nafaka ambayo huhifadhiwa kusaidia katika hali za dharura kama janga la njaa na mahitaji ya kibinadamu.

Kiunjuri Jumatatu akiwa Kirinyaga alisema kuwa kufanya hivyo kutaokoa wakulima wa mpunga kutokana na upenyo wa madalali ambao huvamia maeneo hayo kila wakati wa mavuno na kuishia kusambaratisha uthabiti wa bei.

“Tutaanza kuweka mchele katika mabohari yetu ya kujikinga na upungufu wa chakula. Kwa muda mrefu tumekuwa tukinunua mahindi tu ilihali tunajua kuwa mchele ni nafaka nyingine ambayo inaweza ikahifadhiwa,” akasema.

Alisema kuwa serikali itakuwa ikitangaza bei ya mchele kwa gunia la kilo 50 kila baada ya msimu ili kuwakinga na kushushwa kwa bei na madalali.

“Tukitangaza kuwa kwa mfano gunia hilo litakuwa likinunuliwa na serikali kwa Sh10, itabidi kila mwingine ambaye ako na nia ya kununulia wakulima mchele wao wakae kwa hiyo bei au waizidishe bali sio kuipunguza,” akasema.

Aidha, alisema kuwa wizara yake itajitolea kusaidiana na wakulima hao ili kuzidisha mavuno.

Alisema usaidizi huo utakuwa kupitia kuwapa wakulima hao vifaa muhimu, teknolojia mpya za uzalishaji na kushirikiana katika kupambana na ndege hatari ambao huvamia mashamba ya mpunga na kuzua uharibifu mkuu ambao huishia kuwafukarisha wazalishaji.