Serikali kutumia Sh500m kustawisha masoko ya mifugo

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  10:37

Kwa Muhtasari

Tangazo hili lilitolewa na afisa wa ustawishaji viwanda vya mashinani katika Wizara ya Ugatuzi Bw John Kamuto katika warsha ya wakulima iliyofanyika katika Shamba la Utafiti wa Kilimo la Jomo Kenyatta-Mareira lililopo katika kaunti ya Murang’a.

 

MURANG'A, Kenya

SERIKALI itatumia kitita cha Sh500 milioni kujenga masoko ya mifugo kote nchini kuanzia mwaka ujao.

Masoko hayo yatalenga maeneo ambayo kwa kawaida hayajulikani kwa riziki ya biashara za mifugo ili kuibua mtazamo wa kuekeza katika sekta hiyo miongoni mwa wenyeji.

Masoko hayo yatajengwa katika maeneobunge 35 kwa ushirikiano wa wafadhili, serikali za kaunti na serikali kuu.

Hayo yalisemwa Alhamisi na afisa wa ustawishaji viwanda vya mashinani katika Wizara ya Ugatuzi Bw John Kamuto katika warsha ya wakulima iliyofanyika katika Shamba la Utafiti wa Kilimo la Jomo Kenyatta-Mareira lililopo katika Kaunti ya Murang’a.

Bw Kamuto aliarifu wakulima hao kwamba masoko hayo yatakuwa yakizingatia biashara ya mifugo pekee.

“Kwa sasa, fedha hizo zimetengwa na linalobakia ni kutambua ardhi ambazo zitatumika kujenga masoko hayo. Tunategemea Serikali za Kaunti ambazo zitalengwa kusaidia katika utambuzi wa ardhi hizo,” akasema Bw Kamuto.

Afisa wa ustawishaji wa mifugo katika Kaunti ya Murang’a Bw James Thuo Wainaina alisema kuwa mradi huo utashilikisha Kaunti zilizoko katika maeneo ya Nyanza, Mashariki na Kati.

“Masoko hayo yatajengwa yakizingatia nyanja mbalimbali za sekta ya mifugo ambapo yanaweza yakatumika kuandaa maonyesho ya mifugo ambapo wakulima wanaweza wakajumuika kubadilishana mawazo kuhusu sekta hii,” akasema.

Kuinua wakulima

Bw Wainaina alisema kuwa sekta ya mifugo imeorodheshwa kama kiungo muhimu cha kuafikia mbinu za kuinua wakulima katika ruwaza ya 2030.

Aidha, alisema kuwa masoko ya nje ya bidhaa za mifugo yanaendelea kuimarika hivyo basi kuhimiza serikali ifanye juu chini kuwezesha wakulima kuekeza katika sekta hii jinsi inavyofaa.

Bw Kamuto alisema kuwa hatua hiyo inaenda sambamba na mpango mwingine wa serikali wa kuwafadhili wafugaji kuunda kampuni zao za kuongeza ubora bidhaa.

"Kampuni hizo zinalenga vitengo vya ngozi, maziwa, nyama na mbolea ambapo mradi huo ukifanikiwa kutimizwa utazidisha mapato ya wafugaji kwa kiwango kisichopungua asilima 200," akaongeza Bw Kamuto.