http://www.swahilihub.com/image/view/-/4956528/medRes/2236810/-/rw867xz/-/afyauma.jpg

 

Maafisa wa afya ya umma wa kaunti ya Kiambu wakongamana Thika

Afya ya Umma

Baadhi ya Maafisa wa Afya ya Umma wa kaunti ya Kiambu waliokongamana Januari 29, 2019. Picha/LAWRENCE ONGARO 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Tuesday, January 29  2019 at  12:18

Kwa Muhtasari

Maafisa wa afya ya umma wa kaunti ya Kiambu walikongamana Jumatatu ili kujieleza na vilevile kupewa mafunzo muhimu ya kuboresha utendakazi wao.

 

THIKA, Kenya

MAAFISA wa Afya ya Umma wapatao 60 kutoka Kaunti ya Kiambu wamekongamana Thika kupanga mikakati ya kuboresha utendakazi wao.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya ya Kiambu Bi Mary Kamau, alisema Jumatatu mafunzo ya maafisa hao wa afya ni muhimu kwa sababu italeta sura mpya jinsi ya utendakazi wao katika Kaunti ndogo wanazowakilisha.

"Siku hii ni muhimu sana kwa sababu kila mmoja atajieleza jinsi eneo lake linavyotekeleza wajibu wake na pia ni hatua nzuri ya kubuni mikakati mipya ya kuchapa kazi," alisema Bi Kamau.

Alisema fedha za kugharamia masomo hayo ni udhamini kutoka Benki ya Dunia kwa kitita cha Sh50 milioni kwa kipindi cha miaka mitatu.

Alisema katika awamu ya kwanza watalazimika kutumia takribani Sh7.4 milioni ili kuwapa mafunzo maafisa hao wa afya pamoja na maafisa walio mashinani wa kujitolea.

"Tuna hakika ya kwamba utendakazi mzuri ukiboreshwa na maafisa hawa, bila shaka mwananchi aliye mashinani atanufaika pakubwa kwa kupata huduma kamili. Hilo ndilo lengo letu ya kuona ya kwamba mwananchi ananufaika kiafya," alisema Bi Kamau.

Kupunguza sukari nyingi

Alitoa wito kwa wananchi wabadilishe mtindo wao wa kula chakula ili kupunguza sukari nyingi mwilini na kuzingatia ulaji wa mboga kwa wingi.

"Ulaji mbaya wa chakula ndilo linasababisha maradhi mengi kuandama watu. Kuna maradhi ya saratani, na kuchemka kwa damu mwilini," alisema Bi Kamau.

Bi Susan Waititu ambaye ndiye alikuwa mgeni wa heshima alipongeza mpango huo wa kuwaleta pamoja maafisa wote wa afya ya umma huku akisema ni njia moja ya  kuelewa linalotendeka mashinani.

"Ninawapongeza nyinyi wote kwa kuonyesha jinsi mumejituma kufika kwa ajili ya kupata masomo muhimu kwa kazi yenu," alisema Bi Waititu.

Aliwataka maafisa hao wawe mstari wa mbele kushirikiana kwa pamoja ili kufanikisha malengo yao ya kutendea wananchi haki.

Aliwapongeza maafisa wa mashinani wa kujitolea ambao huhudumia wananchi akisema huo ni mwito na unastahili kuigwa na wengi.