http://www.swahilihub.com/image/view/-/3962792/medRes/1665720/-/851ddr/-/ichamo.jpg

 

Maafisa wa polisi walevi Murang'a wapewa onyo

Naomi Ichami

Naomi Ichami akihutubia mkutano wa wadau kuangazia usalama Juni 8, 2017 katika kanisa la PCEA Murang’a. Picha/MWANGI MUIRURI  

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, December 8  2017 at  08:00

Kwa Muhtasari

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Murang’a, Naomi Ichami, amelalamika akisema visa vya maafisa wengi eneo hilo kuwa walevi kupindukia kiasi kwamba wanatelekeza wajibu wao wa kudumisha usalama vimezidi.

 

KAMANDA wa polisi wa Kaunti ya Murang’a, Naomi Ichami, amelalamika akisema visa vya maafisa wengi eneo hilo kuwa walevi kupindukia kiasi kwamba wanatelekeza wajibu wao wa kudumisha usalama vimezidi.

Amesema ofisi yake imekuwa ikipokezwa malalamishi tele kuhusu maafisa wa polisi ambao wanaonekana wakilewaa kiholela; wengine wakiwa na sare rasmi za kazi katika baa wakiwa wateja wa kawaida.

Katika barua ambayo ametuma kwa makamanda wote wa vituo vya polisi eneo hilo, amesema kuwa afisi yake ingetaka hali hiyo ithibitiwe.

“Ni suala la wazi kwa maafisa wote wa polisi katika Kaunti hii kuwa ni hatia kushiriki ulevi masaa ya kazi na ukiwa na sare rasmi za kikazi,” amesema Ichami.

Ameteta kuwa visa vya maafisa hao walevi kunaswa katika visa vya ukiukaji sheria vimezidi kushuhudiwa, hali ambayo imetia doa nembo ya utenda kazi wa idara ya polisi.

“Kunao pia ambao wameripotiwa kuwa wanachukua magari ya polisi na kuyaegesha nje ya mabaa na maafisa husika wanaingia ndani ya mabaa hayo kuburudika pombe. Hilo ni kinyume na sheria na ambapo ni sawa na utumizi vibaya wa mamlaka na rasilimali za umma,” ameteta.

Amesema kuwa maafisa wengine wanaingiwa na ulevi vichwani mwao na kuwasambaratishia nidhamu za kikazi kiasi kwamba wamegeuka kuwa kero kwa raia.

Amesema kuwa visa vya maafisa wa polisi kunaswa katika vita ndani ya mabaa ya eneo hilo, kashfa za kutisha raia kwa silaha na pia kutoa vitisho vya kukamata raia hao bila msingi wowote vimezidi.

Amewataka makamanda hao kuhakikisha kuwa maafisa wanaohudumu katika vituo vya polisi Murang’a wamewajibikia nidhamu na wale wote ambao ni walevi wamulikwe kisawasawa ili kuokoa idara hiyo aibu za mara kwa mara.