http://www.swahilihub.com/image/view/-/4961820/medRes/2239774/-/g9kstkz/-/ijisha.jpg

 

Maafisa wafanya msako mkali African Spirit Distillers Thika

Musa Yego

Afisa mkuu wa kitengo cha Flying Squad Bw Musa Yego akiwa nje ya kampuni ya African Spirit Distillers Ltd mjini Thika aliponasa mitungi 800 ya kemikali aina ya ethanol. Picha/LAWRENCE ONGARO 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  14:38

Kwa Muhtasari

Kitengo cha jinai cha Flying Squad, na maafisa wa KRA wamefanya msako katika African Spirit Distillers, Thika.

 

THIKA, Kenya

MAAFISA wa kitengo cha jinai cha Flying Squad, na wale wa KRA Alhamisi jioni walivamia kampuni moja ya mvinyo na kuwatia nguvuni mameneja watatukwa kukwepa ulipaji wa ushuru.

Kikundi hicho kilichoongozwa na afisa mkuu wa kitengo cha Flying Squad Bw Musa Yego, na naibu kamishna wa KRA Bi Anne Nyaguthie Irungu, kilipata fununu kutoka kwa wananchi ndipo wakavamia eneo hilo.

Makachero kadha kutoka jijini Nairobi walifanya upelelezi wao ambapo walifuata lori lililobeba bidhaa gushi ambapo lilikamilisha safari yake katika kampuni ya African Spirit mjini Thika.

"Tulipofanya uchunguzi kamili tulipata ya kwamba lori hilo lilitoka nchini Tanzania likiwa limebeba bidhaa gushi. Lakini dereva wake aliposhuku kuwa alikuwa akifuatwa, alitoweka kwa kutumia mlango wa nyuma wa kampuni hiyo," alisema Bw Yego.

Upekuzi uliofanywa ulionyesha ya kwamba kuna mitungi 800 aina ya dramu iliyokuwa kwenye lori hilo huku ikiwa na kemikali ya ethanol.

"Mitungi hiyo ilikuwa imefichwa ndani ya magunia ya mahindi ili isigunduliwe kwa urahisi. Wakati huo pia hawakuwa wamelipia ushuru wa KRA, huku wakikwepa sheria hiyo," alisema Bw Yego.

Pombe

Uchunguzi zaidi unaeleza kuwa kampuni hiyo ya African Spirits Distillers Ltd ndiyo hutengeneza pombe aina ya Blue Moon, na Legends.

Baada ya kufanya upekuzi zaidi maafisa hao walipata lita 10,000 za kemikali aina ya ethanol, na vibandiko bandia vya KRA.

Alisema watazidi kushirikiana na idara ya KRA ili kuona ya kwamba watu wanaofanya mambo kwa njia ya mkato wanatiwa nguvuni.

"Maafisa watatu tuliowanasa wanaendelea kutupatia habari zaidi ili tupate mwelekeo wa kuwafungulia mashtaka," Naibu kamishna wa KRA Bi Irungu alisema na kuongeza kampuni hiyo imekuwa hailipi ushuru na kwa hivyo uchunguzi kamili ukikamilika watafunguliwa mashtaka.

"Tuligundua ya kwamba kampuni hiyo imekuwa ikitumia miigizo gushi kuonyesha ya kwamba vibandiko vyao ni vya KRA," alisema Bi Irungu.

Alitoa wito kwa wananchi wawe mstari wa mbele kushirikiana na polisi ili kufanikisha malengo yao ya kuwanasa wezi wa mali ya umma.

Alisema hatua waliochukua ni ya kupongezwa kwa vile kuna viwanda vingi humu nchini ambavyo vinaendesha mambo yao kwa njia isiyofaa.