NASA: 'Maandamano hutokea kukikosekana demokrasia'

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Saturday, August 12   2017 at  15:37

Kwa Mukhtasari

Seneta wa Siaya James Orengo amesema kuwa wafuasi wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) wanaoandamana mitaani Kibera na Mathare Kaunti na Nairobi na baadhi ya maeneo ya Kisumu, wanatetea haki na hasa kuhakikisha demokrasia inaheshimiwa.

 

SENETA wa Siaya James Orengo amesema kuwa wafuasi wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) wanaoandamana mitaani Kibera na Mathare Kaunti na Nairobi na baadhi ya maeneo ya Kisumu, wanatetea haki na hasa kuhakikisha demokrasia inaheshimiwa.

"Wakati watu hawajaridhishwa na uchaguzi, maandamano hutokea," amesema seneta huyu ambaye ni mmoja wa mawakala wa Nasa, wakati akihutubia waandishi wa habari kwa mara ya kwanza Jumamosi jijini Nairobi, baada ya Rais Uhuru Kenyayta kutangazwa mshindi.

"Maandamano hayo yumkini hayawi ya amani katika kisa kama hicho," amesema.

Kufuatia tangazo la tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kupitia mwenyekiti wake Bw Wafula Chebukati, Ijumaa katika ukumbi wa Bomas of Kenya kuwa Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee ndiye aliibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Jumanne Agosti 8, 2017, muungano wa Nasa ulipinga matokeo hayo na kupelekea wafuasi wake kuanza kuandamana.

Rais Kenyatta na Naibu William wake Ruto ndio wataongoza taifa hili kwa kipindi cha miaka mingine mitano ijayo baada ya kuzoa kura 8,203,290 ikiwakilisha asilimia 54.24 na kinara wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga akipata kura 6,762,224 ikiwa ni asilimia 44.92 kwa jumla ya kura 15,073,662 zilizopigwa na kuwakilisha asilimia 78.91 ya wapiga kura 19,687,563 waliosajiliwa na tume ya IEBC.

Kinara wa Nasa Raila Odinga na vinara wenza walipinga matokeo hayo wakihoji si halali na kwamba yalikumbwa na wizi wa kura.

Bw Kalonzo Musyoka ndiye mgombea mwenza wa Raila.

Seneta Orengo aidha amekashifu mauaji yanayoshukiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi wanaoshika doria katika maeneo yaliyoathirika.

"Hata mtu akiwa mhalifu, anafaa kuuawa kabla hajafikishwa kortini na kupatikana na hatia?" akataka kujua.

Orengo aidha amewataka wafuasi wa Nasa kuwa watulivu. "Tunawaomba muwe watulivu na mjiondoe kwenye njia," akasema.

Wakati huo huo, tume ya kutetea haki za kibinadamu KNCHR imetaka maafisa wa polisi kutotumia nguvu kupita kiasi wakati wanatuliza ghasia. "Maafisa wa polisi wakome kutumia risasi kuimarisha usalama hususan kwa wanaogoma," amesema mwenyekiti wa KNCHR Bi Kagwiria Mbogoria, akihutubia wanahabari kwenye ofisi za tume yake jijini Nairobi na kufichua kuna watu kadhaa wameuawa kwenye maandamano hayo.

Hata hivyo mwenyekiti huyu amewataka waandamanaji huo kufanya maandamano ya amani.

"Kila mmoja ana uhuru kikatiba kushiriki maandamano akitaka haki yake itendeke, lakini yawe ya amani wala si kushambulia watu, kuvunja nyumba na maduka yao na kuiba mali," ameshauri.

Kukanusha

Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i, mapema Jumamosi alikanusha kuwa kuna yeyote ameuawa kupitia maandamano hayo.

"Tulikuwa na mkutano wa usalama na Inspekta Boinnet leo asubuhi (Jumamosi), hakuna jambo kama hilo la mauaji limetokea. Sina habari ya yeyote aliyeuawa kwa kupigwa risasi nchi hii. Nina furaha kwa sababu mnatumia majina 'uvumi unasema' na hatuegemei uvumi ila ukweli," akasema akijibu maswali tata ya wanahabari jijini Nairobi kwamba kuna baadhi ya watu waliouawa kwa kupigwa na maafisa wa polisi, habari ambazo hazijathibitishwa na yeyote.

Alikanusha kuwa maafisa wa polisi wanatumia risasi kutuliza ghasia na maandamano hayo.

"Maafisa wetu wamepokea mafunzo ya kulinda wananchi ila si kuwadhuru. Kumekuwa na uvumi kuwa polisi wanatumia nguvu kutawanya wanaoandamana kinyume cha sheria, huo ni uvumi mtupu," akaeleza.

Akaongeza: "Hakuna afisa wa polisi ambaye amepiga risasi wanaoandamana kwa amani."