Mahojiano yaanza, muungano wa wauguzi waahirisha mgomo Meru

Sehemu ya idara ya kuhudumia majeruhi Meru

Sehemu ya idara ya kuhudumia majeruhi katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Meru mnamo Desemba 5, 2016. Wauguzi Kaunti ya Meru wameahirisha mgomo wao uliotakiwa kuanza Januari 9, 2017. Picha/AGNES ABOO 

Na AGNES ABOO

Imepakiwa - Wednesday, January 11   2017 at  23:44

Kwa Mukhtasari

Mchakato wa kuhoji wafanyakazi wa afya Kaunti ya Meru ili kupandishwa vyeo umeanza baada ya shughuli hiyo kusimamiswa mwaka 2015.

 

MCHAKATO wa kuhoji wafanyakazi wa afya Kaunti ya Meru ili kupandishwa vyeo umeanza baada ya shughuli hiyo kusimamiswa mwaka 2015.

Wakati huo huo muungano wa wauguzi umeamua kuahirisha mgomo wao uliotakiwa kuanza Januari 9, 2017 ili kuipa serikali ya kaunti mUda zaidi wa kutekeleza matakwa yao.

Katibu wa kaunti hiyo Bw Julius Kimathi alisimamisha shughuli hiyo Desemba 8, 2016 kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea nchini licha ya baadhi ya wafanyikazi hao kutoshiriki katika mgomo huo.

Akizungumza Jumatano mjini Meru, Katibu Mkuu wa muungano wa kutetea haki za wauguzi Nchini (Knun) tawi la Meru Bw Nesbit Mugendi alisema kuwa muungano huo uliamua kuahirisha mgomo ili kuipa kaunti muda zaidi wa kutekeleza masuala yao.

“Ni matumaini yangu kuwa masuala yetu yatashughulikiwa kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Januari baada ya kuahirisha mgomo wetu uliyotarajiwa kuanza Jumatatu,” alisema.

Barua

Baadhi ya wafanyikazi wamepata barua za kupandishwa vyeo.

Wale wanohojiwa ni takribani wafanyakazi 800.

Afisa Mkuu wa Afya Kaunti ya Meru Bw James Gitonga alisema kuwa mchakato huo unatarajiwa kukamilika Januari 19 akiongeza kuwa ifikapo mwishoni mwa Januari wale wote watakaofuzu watapandishwa vyeo.

“Tuna wafanyakazi wa afya 833 wanaohojiwa. Serikali ya kaunti imedhamiria kuwa wale wote watakaochaguliwa watapandiswa vyeo mara moja,” alisema Bw Gitonga.