Maiti ya mwanamke yakutwa karibu na lango la shule

Na SAMMY KIMATU

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  13:45

Kwa Muhtasari

Kamanda wa Polisi wa Utawala wa Kaunti ndogo ya Makadara, Superiteni John Macharia amethibitisha kisa hicho.

 

NAIROBI, Kenya

MWILI wa mwanamke asiyejulikana umepatikana karibu na lango la Shule ya Msingi ya St Bakhita iliyopo mkabala na barabara ya Likoni, South B.

Polisi walisema marehemu anakisiwa kuwa aliyekumbana na mauti akiwa kati ya umri wa miaka 18 na 21.

Shingoni mwake alikuwa amefungwa kwa waya unaotumiwa kuunganisha mfumo wa teknolojia ya mawasiliano wa fibre.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Utawala wa Kaunti ndogo ya Makadara, Superiteni John Macharia alisema mwili wa marehemu ulipatika na polisi wa trafiki mwendo wa saa kumi na mbili za asubuhi.

“Hakuwa amevalia viatu, alikuwa na nguo safi licha ya blausi yake kuvaliwa upande wa mbele ukiwa nyuma. Inaonekana aliuliwa kwingineko na akaletwa hapa ionekane alijinyonga usiku,” Sp Macharia akasema.

Utadhani ameketi, kumbe amekufa

Bawabu katika shule karibu ya St Bakhita, Bi Jane Nanjala amesema Jumatano asubuhi mwanamke huyo alionekana kana kwamba ameketi chini akitulia  kwa mtazamo wa mbali lakini ukikaribia ndio utaona waya umefungwa shingoni mwake na sweta ikitupwa karibu na mwili huo chini ya transfoma.

Wanafunzi katika shule ya upili ya St Michael school walijazana juu ya ua wa shule kuuona mwili huo.

SP Macharia aliongeza kwamba mwili ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City.