http://www.swahilihub.com/image/view/-/4186834/medRes/1809524/-/7niesnz/-/nja.jpg

 

Majaji Boma Ojwang, Smokin Wanjala wabadilishana mahali pa kukaa

Jackton Ojwang

Jaji Jackton Ojwang na Jaji Smokin Wanjala wabadilishana pahali wao hukaa wakati wa kusikiza kesi ya pili ya kutaka ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta ubatilishwe na mahakama ya juu zaidi. Picha/RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, November 14  2017 at  17:58

Kwa Mukhtasari

Majaji wawili wa Mahakama ya Juu wamebadilisha pahala pao wanapoketi wakati wa kusikizwa kwa kesi ya kupinga uchaguzi wa pili wa urais mwaka 2017 wa Oktoba 26, 2017.

 

MAJAJI wawili wa Mahakama ya Juu wamebadilisha pahala pao wanapoketi wakati wa kusikizwa kwa kesi ya kupinga uchaguzi wa pili wa urais mwaka 2017 wa Oktoba 26, 2017.

Jaji Smokin Wanjala aliketi karibu na Jaji Njoki Ndung’u.

Kwa kawaida hata nyakati za aliyekuwa Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga ni Jaji Jackton Ojwang anayekaa karibu na Jaji Ndung’u.

Jaji Ojwang alibadilisha mahala  pake na kukaa karibu na Jaji Isaac Lenaola. Awali ni Jaji  Wanjala aliyekuwa anakaa anapokaa Jaji Ojwang.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi ya kwanza mnamo Agosti 2017 Jaji Ndung’u na Jaji Ojwang walikuwa wanakaa upande mmoja n ahata walitofautiana katika uamuzi ulioharamisha ushindi wa Bw Kenyatta.

Hali ya usalama imeimarishwa vilivyo kuanzia Jumanne katika mahakama ya kilele, mandhari na mazingira yake jijini Nairobi, wakati ambapo jopo la majaji saba wa mahakama hiyo wameanza kusikiliza kesi ya kupinga uhalisia wa marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26, 2017.

Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee na wagombeaji wengine watano ndio walishiriki uchaguzi huo baada ya kinara wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga kujiondoa kuushiriki kwa malalamishi kuwa matakwa yake hayakuafikiwa.

Hata hivyo, jina la Waziri huyo Mkuu wa zamani lilikuwa debeni licha ya kujiondoa na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka.

Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto ndio walitangazwa kuibuka washindi kwenye uchaguzi huo, ambao Jaji Mkuu David Maraga anatarajiwa kuongoza jopo lake kusikiliza kesi ya Wakenya watatu wanaopinga uchaguzi huo.

Aliyekuwa mbunge wa Kilome, Harun Mwau, wanaharakati Njonjo Mue na Khelef Khalifa ndio wanapinga uchaguzi huo wakihoji kuwa tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) ilikiuka kanuni za sheria za uchaguzi.

Hata hivyo, Jumatatu Oktoba 30 mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati akitangaza Rais Kenyatta kuibuka mshindi, alisema uchaguzi huo ulikuwa wa huru, haki na wazi na kwamba ulizingatia matakwa ya uchaguzi kama ilivyoagiza mahakama ya kilele wakati ikifuta uchaguzi mkuu wa Agosti 8.

"Uchaguzi wa Oktoba 26, ulikuwa wa huru, haki na wazi. Tulizingatia sheria za uchaguzi kama ilivyoagiza mahakama ya upeo," akasema Chebukati, akihutubu katika ukumbi wa Bomas of Kenya, jijini Nairobi.

Nasa ambayo wiki kadha zilizopita ilibuni vuguvugu la Ukombozi (National Resistance Movement NRM), ilishawishi wafuasi wake wasishiriki uchaguzi huo.

Ngome za Nasa hazikushiriki uchaguzi, kutokana na kudorora kwa usalama ulioshuhudiwa. Hata hivyo, Chebukati alisema matokeo ya maeneo bunge 25 ya kaunti za; Siaya, Homabay, Migori na Kisii yasingeathiri ushindi wa Rais Kenyatta.

"Kura za maeneo bunge hayo hazitaathiri ushindi wa Bw Uhuru Kenyatta, kwa hivyo hatuna budi kumtangaza mshindi," akasema Chebukati.

Muungano wa Nasa, aidha umepinga uchaguzi huo ukitaka serikali ya mpito ibuniwe na kuhudumu kwa miezi 6 ijayo ili uchaguzi mpya uitishwe. Hata hivyo, Jubilee inasema njia pekee ya yeyote kuwa mamlakani sharti ashiriki uchaguzi.

Nasa inashinikiza pendekezo lake kwa kushawishi wafuasi wake wapuuze bidhaa na huduma za baadhi ya kampuni wanazosema zinaunga mkono Jubilee.

Nasa pia iko katika harakati za kubuni mabunge ya mwananchi katika kaunti ngome zao, yenye malengo ya kumng'atua Rais Kenyatta endapo mahakama ya kilele itafutilia mbali kesi za Wakenya hao watatu wanaopinga uhalali wa Oktoba 26.

Kando na Wakenya hao, Taasisi ya Democratic Governance imewasilisha kesi yake katika mahakama hiyo, ikimtaka kinara wa Nasa Bw Raila kufunguliwa mashtaka kwa kukiuka sheria za uchaguzi ikikumbukwa kwamba yeye ndiye aliwasilisha kesi katika mahakama hiyo ya kupinga uchaguzi wa Agosti 8.

Maafisa wa usalama wameonekana wakishika doria katika kitovu cha jiji la Nairobi (CBD).

Hata hivyo, maafisa hao si wengi kama ilivyotarajwa ikilinganishwa na wa kesi ya kufutilia mbali uchaguzi wa Agosti 2017.

Katika uamuzi wa Septemba 1, 2017 Jaji Mkuu (CJ) David Maraga, naibu wake (DCJ) Philomena Mwilu, Wanjala na Lenaola walikubaliana kwamba uchaguzi wa Bw Kenyatta haukuwa wa haki.

Jaji Mohammed Ibrahim ni mgonjwa na yuko ng’ambo akipokea matibabu.