http://www.swahilihub.com/image/view/-/4186504/medRes/1809314/-/s0oodxz/-/furika.jpg

 

Maji ya mafuriko ni kadhia kwa wafanyabiashara Makongeni

Makongeni

Sehemu ya soko la Makongeni lililoko Wadi ya Kamenu, Thika iliyoathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua Novemba 13, 2017. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, November 14  2017 at  14:38

Kwa Muhtasari

Soko la Makongeni, Thika lililoko kwenye barabara ya Thika-Mwingi limegeuka uwanda wa maji kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha maeneo hayo.

 

SOKO la Makongeni, Thika lililoko kwenye barabara ya Thika-Mwingi limegeuka uwanda wa maji kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha maeneo hayo.

Aidha soko hilo ni miongoni mwa masoko tajika katika kaunti ya Kiambu yanayouza bidhaa za kula na vilevile nguo, viatu na bidhaa zingine.

Kufuatia mvua iliyonyea wikendi, wafanyabiashara wengi hususan wa maeneo yaliyoathirika pakubwa hawakuweza kufungua kazi zao mnamo Jumatatu na Jumanne.

Swahili Hub ilipozuru soko hilo jana ilithibitisha hali haikuwa hali tena kutokana na mafuriko yaliyosomba hata baadhi ya vibanda vinavyomilikiwa na wauzaji.

Aidha ilikuwa vigumu kwetu hata kuingia sokoni, kwa kuwa maji yalikuwa mithili ya yale ya kidimbwi.

Sehemu inayouzwa bidhaa za kula ndiyo iliathirika pakubwa, huku wanaouzia maeneo hayo wakisalia na kilio; 'Nani atakayekiskia kilio chetu ilhali viongozi tuliochagua wametupuuza?'

Bi Ann Njeri muuzaji wa machungwa alisema juhudi za kufikia viongozi waliowachagua serikalini hazikuzaa matunda yoyote, kwa sababu hawakujibu arafa walizotumiwa wala kupokea simu.

"Sisi hutegemea soko hili kulisha familia zetu, tulipofika hapa asubuhi halikuwa likiingilika kwa sababu ya mafuriko. Gavana wa Kiambu, mbunge wa Thika, diwani walipokuwa wakiomba kura walituahidi kuunda upya soko hili. Kwa sasa hata jumbe hawarejeshi, simu hawapokei," akateta Bi Njeri, kwenye mahojiano ya kipekee.

Ferdinand Waititu ndiye gavana wa Kiambu, mbunge wa Thika ni Wainaina wa Jungle. Soko hilo liko katika Wadi ya Kamenu, na MCA wake ni Bw Raphael Chege.

"Wakiomba kura walikuwa wakija hapa kila siku wakitupa ahadi chungu nzima, kwa sasa hawaonekani tena. Hii si haki, Wanjiku apewe haki yake," akasema Bi Njeri.

Kibanda kusombwa

Bi Mercy Wanjiru anayeuza vitunguu hakuweza kufungua biashara yake akisema alipoamkia gange asubuhi alipata kibanda chake kimesombwa na maji.

"Leo watoto wangu watakula wapi kwa sababu sijafungua kazi?" akataka kujua Bi Wanjiru.

Wafanyabiashara tuliozungumza nao walinyooshea viongozi wao kidole cha lawama, wakiteta kuwa tangu wachaguliwe hawajawahi zuru Soko hilo.

"Tangu tuwape kura hawaji tena, roho zao hazipo Thika. Ahadi tele walizotupa zimepuuzwa sasa, hawazungumzi kuzihusu hata tunawaona kwenye runinga tu. Hata kuja kutupa matumaini pekee hawaji. Agosti 8, uliamka asubuhi na mapema kuwachagua, wako wapi sasa?" akataka kujua Bw Francis Waweru, muuzaji wa viazi mbatata.

Soko hilo lilivyoathirika na mafuriko ni hatari kwa usalama wao binafsi, hususan kuambukizwa ugonjwa wa Kipindupindu kwa kuwa asilimia kubwa ni ya bidhaa ni za kula.

Walieleza kuwa mboga aina ya kabeji zilizoletwa na malori na kupakuliwa Jumapili usiku, kuamkia asubuhi ya jana nyingi yazo zilikuwa zimesombwa.

"Asubuhi kabeji nilizopata zinahesabika ilhali zilikuwa lori nzima, hii ni hasara tupu," akateta Mwalimu Mburu.

Alisema miezi mitatu tangu uchaguzi mkuu wa Agosti 8, ufanyike ni kipindi kirefu ambacho soko hilo lingekuwa limeundwa upya na viongozi waliowachagua.

Alinyooshea kidole cha lawama MCA wa wadi ya Kameno, akisema hilo ni jukumu lake kufahamisha gavana wa Kiambu masaibu kama hayo ili yarekebishwe.

"Kazi ya ugatuzi ni kuunda soko kama hili, hii ni kazi ya MCA," akasema.

Kingo za mitaro ya kusafirisha maji taka aidha zilifuja.

"Mitaro ya maji taka ni duni, hatuna sehemu za kujikinga jua wala mvua," akadokeza Bw Waweru.

Takriban robo tatu ya wafanyabiashara wa Soko la Makongeni hawajaweza kurejelea kazi zao, kutokana na hali mbaya ya mafuriko hayo.

Nyumba za wakazi wa Thika pia hazikusazwa na mafuriko hayo, yakionesha hatari zinazowakodolea macho endapo hali hiyo haitaangaziwa.

Hadi tulipofikia wakati wa kuchapisha habari, jumbe tulizotumia baadhi ya viongozi waliochaguliwa eneo hilo hazikuwa zimerejeshwa.

Mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE unaoendelea, maafisa wa polisi wanalazimika kusafirisha watahiniwa wa shule zilizoathirika kwa magari yao.

Watabiri wa hali ya anga wanasema mvua kubwa inayonyea sehemu mbalimbali nchini, itaendelea hadi mwezi Desemba.