http://www.swahilihub.com/image/view/-/4395630/medRes/1940450/-/4cfi7b/-/nkatha.jpg

 

Makamishna watatu wajiuzulu IEBC

Consolata Nkatha-Maina

Consolata Nkatha-Maina ambaye amekuwa Naibu Mwenyekiti wa IEBC amejiuzulu Jumatatu, Aprili 16, 2018, pamoja na makamishna Paul Kurgat na Margaret Mwachanya. Picha/MAKTABA  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  09:17

Kwa Muhtasari

Mzozo unaoendelea kushuhudiwa katika tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) umeonekana kuchukua mkondo tofauti baada ya makamishna watatu kujiuzulu Jumatatu.

 

MZOZO unaoendelea kushuhudiwa katika tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) umeonekana kuchukua mkondo tofauti baada ya makamishna watatu kujiuzulu Jumatatu.

Kwenye taarifa ya pamoja, naibu mwenyekiti Consolata Nkatha-Maina, makamishna Paul Kurgat na Margaret Mwachanya wamemnyoosheakidole cha lawama mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati wakisema ameshindwa kuongoza tume hiyo na kuleta mshikamano unaofaa.

Taarifa hiyo iliyosomwa na kamishna Mwachanya inasema kuna maswala mengi yaliyopuliziwa kipenga ili yaangaziwe lakini Chebukati hakuchukua hatua yoyote kuyatatua.

"Unapoona kiongozi kama mimi anachukua hatua ya kujiuzulu kuna sababu maalum ambazo tumejaribu kueleza lakini hazijaangaziwa," akasema Bi Mwachanya kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi mnamo Jumatatu.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa IEBC inaendelea kusambaratika chini ya Chebukati, ikionekana kugawanyika kwa misingi ya kisiasa na ubinafsi. Inaongeza kwamba mwenyekiti huyo amekosa kuwa na msimamo dhabiti.

"Tulipoingia ofisini, tuliapa kufanya kazi kwa uwazi na uaminifu haiwezekani kuwe na mvutano kati ya mwenyekiti na naibu mwenyekiti.Tume inaendelea kusambaratika huku maswala yetu ya ndani kwa ndani, hasa yale muhimu yakifichuka. Kuna ushawishi wa kisiasa ndani ya IEBC," akasema Mwachanya kwenye taarifa hiyo.

Siku kadha zilizopita, tume hiyo imekuwa kwenye mizani ya ufujaji wa fedha kufuatia uchaguzi mkuu wa 2017 na 2013. "Chini ya uongozi wa mwenyekiti, tume imekuwa ugani wa utumizi mbaya wa fedha," akaeleza Mwachanya.

Mahakama yakataa

Wiki iliyopita, Chebukati alimpa likizo ya lazima afisa mkuu mtendaji Bw Ezra Chiloba akimtuhumu kuhusika na masaibu yanayokumba IEBC. Afisa huyo aliwasilisha malalamishi yake mahakamani ili kumzuia kufurushwa lakini mahakama ilidinda kuridhia pendekezo lake.

Hatua hiyo ilisababisha migawanyiko zaidi katika IEBC ambapo makamishna waliojiuzulu waliripotiwa kuegemea upande wa Chiloba. Waliomuunga Chebukati ni Boya Molu na Profesa Abdi Guliye.

Kulingana na watatu hao, hatua ya kumtimua Chiloba ni swala linalofaa kuchukuliwa kwa uzito.

Mgawanyiko sawa na huo ulishuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8 mwaka uliopita. Itakumbukwa kwamba kabla ya marudio ya Oktoba 26, kamishna Dkt Roselyn Akombe alijiuzulu kwa madai ya baadhi ya makamishna wa IEBC kuegemea mirengo ya kisiasa.

Bi Nkatha hata hivyo, ametetea utendakazi wao akisema uchaguzi mkuu na marudio ya urais yalikuwa ya huru, haki na wazi.

Hatua ya makamishna hao kujiuzulu ghafla imejiri wakati ambapo Chebukati alitarajiwa kufanya mkutano wa dharura nao baadaye Jumatatu.