Maspika wa kaunti wanataka Seneti izuie kutimuliwa kwao

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  13:05

Kwa Muhtasari

Maspika wanahisi seneti ikiwa na sauti ya mwisho, bila shaka patakuwepo utulivu - hasa likija suala la kutimuliwa kwao.

 

NAIROBI, Kenya

MASPIKA wa mabunge ya kaunti sasa wanataka Bunge la Seneti liwe na usemi wa mwisho katika mchakato wa kuwatimua afisini kama njia ya kuleta utulivu katika mabunge hayo.

Muungano wa Maspika wa Mabunge ya Kaunti (County Assemblies Forum, CAF) Jumatano ulilalamikia maseneta kwamba wakati huu maspika wanakabiliwa na tisho kuu kutoka kwa madiwani hali ambayo inahujumu utendakazi wao na shughuli za mabunge ya kaunti kwa jumla.

Mwakilishi wa CAF Bw Joshua Kiptoo aliyefika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Haki na Masuala ya Sheria aliwataka maseneta hao kuwakinga Maspika hao ambao hawana majukwaa ya kuwasilisha malalamishi yao isipokuwa mahakamani.

"Kama njia ya kuokoa hali, hoja za kuwatimua maspika wa mabunge ya kaunti zinapasa kuwasilishwa kwa seneti kama inavyofanya kuhusu hoja za kuwaondoa afisini magavana," akasema Bw Kiptoo ambaye pia ndiye Spika wa Bunge la Kaunti ya Nandi.

Bw Kiptoo alisema madiwani wamekuwa wakitumia vibaya sheria za mabunge yao ambazo wamekuwa wakizifanyia mabadiliko kwa lengo la kuwatimua maspika wao bila sababu maalumu.

"Mahakama nazo hazijaweza kusaidia kumaliza mizozo katika mabunge ya kaunti na ndio maana tunaomba Seneti kuingilia kati," akasisitiza.

Mabunge mengi ya kaunti yamekuwa yakikumbwa na misukosuko huku maspika wakitumuliwa, hali ambayo imeibua hofu kwamba huenda manufaa ya ugatuzi yakakosa kuafikiwa.

Baadhi ya kaunti

Baadhi ya kaunti ambazo zimekuwa na songombingo na kusababisha kutimuliwa kwa maspika ni Kisumu, Nairobi, Kakamega, Nyandarua na Homa Bay.

Bw Kiptoo alidai kuwa baadhi ya magavana ndio wanachochea hoja za kutimuliwa kwa maspika.

"Kama wewe ni spika na haufuati maagizo ya gavana, huwa anashirikiana na Madiwani ili kuandaa mpango wa kuondolewa kwa spika kama huyo afisini," akasema.

Aliongeza kuwa maspika wanaolenga ni wale ambao wamekuwa wakikemea ufisadi uliokithiri katika kaunti zao, hali ambayo huwakera magavana.

"Wadhifa wa Spika wa Kaunti ulibuniwa na Madiwani na ndio maana tunalazimishwa kuwatii kila wakati. Tunaishi siku moja ikiwa hatuna uhakika kama tutahifadhi kazi yetu siku inayofuta. Hatuwezi kufanya maamuzi kwa njia huru na itakayoweza kufaidi mabunge tunayoongoza na serikali husika za kaunti," Spika Kiptoo akalalamikia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei.

Alisema ingawa sheria inasema kuwa hoja ya kumtimua Spika sharti iungwe mkono na madiwani wasiopungua thuluthi moja, Bw Kiptoo alisema madiwani wamekuwa wakibadili sheria za mabunge yao ili kukimu matakwa yao.

"Katika hali ambapo kazi zetu sio salama, baadhi yetu hulazimika kutii magavana ili kujikinga dhidi ya hatari ya kufutwa kazi na madiwani wandani wa wakuu hao wa kaunti," akaeleza.

Bw Cherargei alimhakikishia Bw Kiptoo kwamba seneti itaingilia kati masaibu yao kwani wajibu wake mkuu ni kulinda ugatuzi.

"Ikiwa mwalengwa kimakosa, Seneti haitasita kuwasaidia. Hii ni kwa sababu hatutaki ugatuzi uathirike kwa njia yoyote kwa sababu ya matakwa finyu ya watu wachache.," akasema huku akiongeza kuwa maspika wanapaswa kufanya kazi katika mazingira tulivu.

Seneta wa Nakuru Susan Kihika aliyataka mabunge ya kaunti kuangazia majukumu yao ya kutunga sheria na kuchunguza utendekazi wa serikali zao badala ya kushiriki vita na fujo za kila mara.