http://www.swahilihub.com/image/view/-/4844594/medRes/2165564/-/ik2x53z/-/uhulia.jpg

 

Viongozi serikalini, upinzani wahudhuria mazishi ya babake Kalonzo

Tseikuru

Rais Uhuru Kenyatta akitoa salamu za rambirambi Novemba 9, 2018, katika mazishi ya Mzee Peter Musyoka Mairu, babake mwanasiasa Kalonzo Musyoka na ambayo yalifanyika Tseikuru, Kaunti ya Kitui. Picha/PSCU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  17:45

Kwa Muhtasari

Mzee Peter Kalonzo Mairu aliyefariki Oktoba 28, 2018, amezikwa Ijumaa katika eneo la Tseikuru, Kaunti ya Kitui.

 

KITUI, Kenya

RAIS Uhuru Kenyatta, Ijumaa aliongoza taifa katika kumuaga baba ya kiongozi wa Wiper Party Kalonzo Musyoka, Mzee Peter Kalonzo Mairu aliyefariki Oktoba 28, 2018.

Marehemu amezikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Tseikuru, Kalimani, kaunti ya Kitui.

Mbali na Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, spika wa bunge la seneti Ken Lusaka, kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale, kiongozi wa wengi seneti Kipchumba Murkomen, kiongozi wa wachache katika seneti James Orengo, mawaziri, magavana, na maseneta, ni baadhi ya viongozi wakuu serikalini na upinzani waliohudhuria mazishi ya mwendazake.

Siasa zimetawala hafla ya mazishi ya Mzee Mairu.

Rais Kenyatta alirejelea mapatano yake na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ya hapo Machi 9, 2018, maarufu kama handshake.

Kiongozi huyu wa taifa alisema sababu hasa ya wawili hao kufanya salamu za maridhiano ilikuwa kuunganisha taifa, kuondoa ukabila na kufanikisha maendeleo kwa kila Mkenya.

"Tulijua kuwa tukilumbana wanaoumia ni wananchi wa Jamhuri hii ya Kenya. Sisi kama viongozi hatutaruhusu tena umwagikaji wa damu, Wakenya kupoteza mali yao na kudororesha uchumi," alisema Rais Kenyatta.

Uhuru

Kenyatta amemtaka kila Mkenya kujihisi huru kutembea na kuishi sehemu yoyote ile ya taifa.

"Kila mmoja ana uhuru wa kuenda popote atakapo kuomba kura kwa kuwa umoja na utangamano ndizo nguzo zetu. Ninaomba viongozi wengine waje tusaidiane kupambana na ufisadi," alieleza kiongozi wa nchi.

Kauli ya Kenyatta kuhusu Handshake iliwiana na ya Naibu wa Rais William Ruto.

"Nafasi tuliyonayo sasa si ya siasa, viongozi wala nyadhifa ila ni ya maendeleo kwa Wakenya. Mapatano yalikuwa ya kuleta maendeleo nchini," alisema.

Aidha, Ruto aliisifia serikali ya Jubilee huku akiorodhesha miradi ya maendeleo iliyofanywa Kitui.

Raila wakati akitoa salamu zake, amesema handshake ililenga kumaliza ukabila, ufisadi, utovu wa usalama, kama vigezo vikuu.

Raila amekemea malumbano yanayoshuhudiwa katika mabunge ya kaunti, akisema yameipa Kenya sifa mbaya katika mataifa ya kigeni.

"Mizozo tunayoona kati ya madiwani (MCA) na maspika imeharibia Kenya jina kule nje. Hakuna anayetaka kuona mwakilishi wa nchi hii katika mataifa hayo," alieleza Raila. Katika siku za hivi karibuni, madiwani wameonekana kuzozana na maspika wa kaunti. Kaunti ya Nairobi na Homa Bay ndizo za hivi punde kuwa na mzozo.

Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi alimpongeza Rais Kenyatta katika juhudi zake katika vita dhidi ya ufisadi. Alisema suala la ufisadi ndilo limelemaza maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na kunyima vijana nafasi za ajira.

Kenya inasemekana kudaiwa zaidi ya Sh5 trilioni, na Mudavadi amemhimiza Rais kutafuta njia za kudhibiti madeni yanayoendelea kuongezeka.

"Tunakuomba utuokoe kutoka kwa madeni," alisema. Hata hivyo, Rais Kenyatta alitetea hatua ya serikali kukopa akisema fedha hizo ndizo zinatumika kufanya maendeleo.