http://www.swahilihub.com/image/view/-/4020450/medRes/1705023/-/tsmax1z/-/ged.jpg

 

Askofu Kairu: Mungu ajua mbona ikawa ni Uhuru Kenyatta

Peter Kairu

Askofu Peter Kairu. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, December 8  2017 at  06:34

Kwa Muhtasari

Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki, Peter Kairu, amewataka Wakenya waungane pamoja kwa hiari na wajiepushe na siasa za kuchukiana.

 

ASKOFU mstaafu wa Kanisa Katoliki, Peter Kairu, amewataka Wakenya waungane pamoja kwa hiari na wajiepushe na siasa za kuchukiana.

Amesema kuwa hali ya sasa ya taifa kupata rais aliyeidhinishwa kisheria ni usemi wa Mungu kupitia wateule wake ndani ya jumuia ya wapiga kura na hatimaye maafisa wa idara za IEBC na mahakama ya upeo ambapo jina la rais Uhuru Kenyatta liliishia kuwa la kuapishwa kuwa rais wa Kenya.

Akiongea Mjini Nyeri, Kairu alisema: "Kile tu kimebakia ni wale ambao wako na maoni kuwa rais Kenyatta hakustahili kuchaguliwa waelewe kuwa msingi wa demokrasia huwa hivyo.”

Amesema kuwa Mungu kwa haki yake alijua nani atakuwa rais katika kipindi cha 2017 hadi 2022 hata kabla ya wapiga kura wajipange kushiriki shughuli hiyo.

Alisema kuwa Mungu kwa busara yake mwenyewe anajua ni kwa nini iwe ni rais Kenyatta mamlakani wala sio mwingine yeyote kati ya wote wanane waliokuwa wakiwania urais katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017 na ule wa marudio wa Oktoba 26, 2017.

Kairu amesema kuwa huo ndio uamuzi wa kuheshimiwa lakini wa kuombewa utilie makini sana umoja wa taifa hili na watu wake wastawi kimaisha.

Amesema kuwa umoja wa kitaifa ni suala muhimu sana kuliko masuala mengine yoyote kwa kuwa umoja huo ndio utazua usalama kwa wote na usalama huo uwe msingi wa kimaendeleo.

Amesema kuwa yeye binafsi hatachoka kila saa kuomba Mungu azidishie taifa hili Baraka za usalama na umoja wa watu wake ili katika kuishi maisha yao hapa nchini, wawe wa kutii kuwa kuna Mungu ambaye ni mratibu wa yote ya kila siku hapa nchini.

Kairu amesema kuwa Mungu yuko na Kenya na watu wake kwa ujumla na yote yataishia kuwa salama kwa jina lake tukufu.