http://www.swahilihub.com/image/view/-/2813218/medRes/1075850/-/p8opalz/-/DNNURSES2505A.jpg

 

Mgomo wa wauguzi wanukia kaunti 24 nchini Kenya

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) Seth Panyako

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) Seth Panyako akihutubia wanahabari Mei 25, 2015. Picha/EVANS HABIL 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  15:35

Kwa Muhtasari

Mgomo wa wafanyakazi katika idara ya afya si jambo geni nchini Kenya.

 

NAIROBI, Kenya

MWAKA hauishi aghalabu bila ya madaktari, matabibu au wauguzi kutishia kushiriki mgomo kwa kile kinachotajwa kama serikali kukosa kuafikia matakwa yao.

Muungano wa kitaifa wa wauguzi nchini (KNUN) Jumatano umetangaza kwamba wauguzi wa kaunti 24 wataweka chini zana zao za kazi kuanzia Jumatatu ijayo.

Katibu mkuu wa muungano huo Seth Panyako amesema kaunti hizo hazijalipa wauguzi wake marupurupu kwa mujibu wa mkataba KNUN ilitia saini na serikali Novemba 2, 2017.
Miongoni mwa kaunti ambazo huduma za afya zitaathirika ni; Kwale, Kirinyaga, Marsabit, Embu, Mandera, Nyandarua, Wajir, Homa Bay, Murang'a na Taita Taveta. Kwenye kikao na waandishi wa habari jijini Nairobi, Dkt Panyako amesema kaunti tatu pekee ndizo zimeheshimu mkataba huo na kwamba huduma za matibabu humo hazitaathirika.

Kaunti hizo ni; Machakos, Migori na Mombasa.

Amesema Hazina ya Kitaifa kwenye makadirio yake ya bajeti mwaka wa fedha 2018/2019, wauguzi walitengewa mshahara wao pamoja na marupurupu kwa mujibu wa mkataba wa 2017 na fedha zikatumwa katika serikali za kaunti lakini tume ya kuainisha mishahara ya watumishi wa umma (SRC) ndiyo imekuwa kizingiti kikuu.

"Tunajua pesa zilitolewa na hazina ya kitaifa, serikali za kaunti zimekataa kulipa wauguzi marupurupu yao kwa madai kuwa SRC haijatoa mwelekeo. Hayo hatutakubali, tunataka tume hiyo iondolewe kwa sababu imeleta mambo mabaya kwa wafanyakazi wa Kenya, inanyanyasa sana," amelalamika Dkt Panyako.

Amesema kaunti 20 zimeonesha dalili ya kulipa wauguzi wake marupurupu, akionya ikiwa kufikia mwezi Machi mwaka huu wauguzi hawatakuwa wamelipwa KNUN haitakuwa na budi ila kuwashawishi wafanye mgomo.
Mwaka wa 2017, wauguzi walishiriki mgomo wa kitaifa uliodumu miezi mitano. Shughuli za matibabu ziliathirika pakubwa, ambapo wagonjwa kadhaa waliripotiwa kufariki.