Polisi Busia wamsaka mshukiwa wa unajisi

Na GAITANO PESSA

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  13:14

Kwa Muhtasari

Mwanamume mwenye umri wa miaka 45 anasakwa na maafisa wa polisi baada ya kufumaniwa na mkewe akimnajisi mwajiri wake katika mkahawa mmoja eneo la Kemodo, eneobunge la Teso Kusini katika kaunti ya Busia.

 

BUSIA, Kenya

MWANAMUME mmoja mwenye umri wa miaka 45 anasakwa na maafisa wa polisi baada ya kufumaniwa na mkewe akimnajisi mwajiri wake katika mkahawa mmoja eneo la Kemodo, eneobunge la Teso Kusini katika kaunti ya Busia.

Mfanyakazi huyo mwenye umri wa miaka 17 amehudumu katika mkahawa huo unaomilikiwa na mshukiwa kwa majuma mawili.

Mshukiwa yuko mafichoni.

Kisa hicho cha Alhamisi alfajiri kimethibitishwa na kaimu chifu wa kata ya Ochude William Egesa aliyefichua kuwa mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Ben mwenye wake wawili amekuwa na mazoea ya kuwadhulumu kimapenzi wafanyakazi wake wa mkahawani.

“Alimwamusha mfanyakazi saa kumi asubuhi kuanza shughuli za kuandaa chakula katika mkahawa kabla ya kumparamia. Hata hivyo, mkewe aliyekuwa amepashwa habari na mwathiriwa aliwafuata na kumfunia 'mzee wake' akimtendea unyama msichana huyo kabla ya mshukiwa kutokomea,” amesema Bw Egesa.

Ameongeza kuwa wameanzisha msako kwa ushirikiano na polisi ili kumnasa, kumtia mbaroni na kumfungulia mashtaka.

“Hii ni mara ya pili mshukiwa kumdhulumu msichana huyo kwa kipindi cha juma moja. Nilimueleza afike hospitalini na kupiga ripoti kwa polisi tunapoendeleza uchunguzi wa kumsaka mafichoni,” amefichua.