http://www.swahilihub.com/image/view/-/4566602/medRes/1976161/-/4qtqba/-/ramua.jpg

 

Sekondari ya Bujra yafungwa uchunguzi wa kiini cha moto ufanywe

Bujra

Wanafunzi wa shule ya wavulana ya Lamu Bujra wajiandikisha kabla ya kutoka shuleni Alhamisi, Mei 17, 2018, baada ya shule hiyo kufungwa kwa muda usiojulikana kufuatia visa vya wanafunzi kuchoma mabweni. Picha/KALUME KAZUNGU 

Na KALUME KAZUNGU

Imepakiwa - Thursday, May 17  2018 at  14:45

Kwa Muhtasari

Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Lamu Bujra imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia visa vitatu vya moto katika kipindi cha wiki moja pekee.

 

SHULE ya Sekondari ya Wavulana ya Lamu Bujra imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia visa vitatu vya moto katika kipindi cha wiki moja pekee.

Akitoa tangazo hilo muda mfupi baada ya kikao kilichowakutanisha wasimamizi wa shule na wadau mbalimbali wa elimu Alhamisi, Afisa Msimamizi wa Masuala ya Elimu, Kaunti ya Lamu, William Micheni, amesema wameafikia kuifunga shule hiyo ili kutoa mwanya wa uchunguzi kufanywa kuhusiana na visa vya mara kwa mara vinavyoshuhudiwa vya mabweni kuchomwa shuleni humo.

Jumatano, mali ya mamilioni ya fedha iliteketea pale moto ulipozuka katika bweni moja kwa jina Mamba shuleni humo.

Bw Micheni amesema wazazi watajulishwa tarehe ya shule hiyo kurejelea masomo punde uchunguzi utakapokamilika.

“Baada ya mkutano na wadau wa elimu, ikiwemo wazazi na wasimamizi wa shule, tumeafikia kuifunga shule kwa muda usiojulikana ili kupisha uchunguzi. Tutawajulisha baadaye tarehe ya kufunguliwa kwa shule. Kwa sasa wanafunzi wote mwende nyumbani,” akasema Bw Micheni.

Kisa hicho pia kimethibitishwa na Mwenyekiti wa Shule hiyo ambaye pia ni Chifu wa Mkomani, Bw Masjid Basheikh.

“Waende nyumbani lakini uchunguzi bado unaendelea. Atakayepatikana ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” akasema Bw Basheikh.

Wanafunzi kukamatwa

Mapema Alhamisi, wanafunzi watatu walikamatwa na polisi kwa kukisiwa kuhusika na uchomaji wa shule.

Magodoro 50, vitanda, masanduku na nguo ni baadhi ya vitu vilivyoteketea wakati wa mkasa wa moto wa Jumatano jioni japo hakuna aliyefariki wala kujeruhiwa wakati wa tukio hilo.

Mnamo Jumapili usiku, chumba cha kiranja wa shule hiyo kiliunguzwa moto katika kisa kinachokisiwa kuwa cha wanafunzi.

Mnamo Alhamisi wiki jana, magodoro 40, vitanda na masanduku ya wanafunzi viliteketea kwenye mkasa wa moto katika bweni kwa jina Zambarani shuleni humo.