http://www.swahilihub.com/image/view/-/2850168/medRes/1104816/-/ng3oxcz/-/DNCOASTDP2508J.jpg

 

Ruto: Siasa za chuki na ukabila hazina nafasi Kenya

William Ruto

Naibu Rais William Ruto akihutubu awali. Picha/WACHIRA MWANGI  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Monday, January 28  2019 at  08:04

Kwa Muhtasari

Rais Uhuru Kenyatta amemkumbatia mpinzani wake mkuu kisiasa, Raila Odinga.

 

KAJIADO, Kenya

NI wajibu wa kila kiongozi na Mkenya kuhakikisha taifa limesonga mbele.

Naibu Rais William Ruto amesema maendeleo yataafikiwa endapo Wakenya, kuanzia viongozi hadi wananchi watashirikiana.

Dkt alisema maendeleo hayatafanyika iwapo utangamano na umoja miongoni mwa wananchi hautakuwepo. Akiongea baada ya kushiriki ibada ya kanisa Ngong, Kajiado, Jumapili Naibu Rais alisema msimu wa siasa uliisha mwaka 2017, akisisitiza kwamba huu ni wakati wa maendeleo ili taifa lisonge mbele.

Licha ya wakosoaji wa Dkt Ruto kudai ziara zake maeneo mbalimbali nchini akizindua miradi ya maendeleo na kukagua iliyoanza awali ni njia ya kufanya kampeni za 2022, kiongozi huyu alisema kibarua kilichoko kwa sasa ni kuhudumia Wakenya ila si kuchapa siasa za urithi.

Alisema serikali ya Jubilee imevalia njuga kuafikia ajenda kuu nne za Rais Uhuru Kenyatta ili kuona Kenya imepiga hatua mbele. Ajenda hizo ni; ujenzi wa viwanda, afya kwa wote, makazi bora na nafuu na usalama wa chakula.

"Tuna taifa ambalo tunapaswa kulisukuma mbele. Huu ni wajibu tunaofaa kushirikiana," alisema Dkt Ruto.

Kauli yake imejiri wiki moja baada ya Rais Kenyatta kumteua waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang'i kama mwenyekiti wa kamati simamizi ya miradi yote ya serikali na mawaziri, wadhifa unaochukuliwa sawa na wa waziri mkuu.

Uteuzi huo umezua tumbojoto kwa wandani wa Naibu Rais, wakiona kana kwamba Ruto amenyang'anywa majukumu yake.

Hata hivyo, Ruto ametangaza kuunga mkono uteuzi wa Matiang'i.

Handisheki

Machi 2018 Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walikubaliana kuunganisha taifa kupitia salamu za mariadhiano maarufu March Handshake. Bw Ruto akirejelea maafikiano hayo, alisema ni hatua ambayo ilileta upinzani pamoja na serikali ya Jubilee ili kuzika katika kaburi la sahau uhasama wa kisiasa kwa minajili ya kuwafanyia Wakenya maendeleo.

"Ndio maana tulileta upinzani pamoja ushirikiane na serikali ili tuwache siasa za chuki, ukabila, utengano na uhasama, tufanye maendeleo," alieleza.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakidai aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga anashirikiana na Jubilee kuvuruga mahesabu ya Ruto ya mwaka wa 2022 ili kuzima ndoto yake kumrithi Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Raila mara kwa mara amekuwa akimsuta Naibu Rais kuwa tayari amenza kufanya siasa za urithi, suala analosema linaweza likahujumu maendeleo.