AU: Uchaguzi Kenya haukuwa na doa lolote

Thabo Mbeki

Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki anayeongoza ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Kenya, ahutubu Julai 22, 2017 katika hoteli ya Intercontinental, Nairobi. Picha/EVANS HABIL 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, August 10  2017 at  11:53

Kwa Mukhtasari

Muungano wa Afrika (AU) umepongeza tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kwa jinsi ilivyoendesha uchaguzi mkuu mnamo Jumanne Agosti 8, 2017.

 

MUUNGANO wa Afrika (AU) umepongeza tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kwa jinsi ilivyoendesha uchaguzi mkuu mnamo Jumanne Agosti 8, 2017.

Akitoa ripoti ya AU kuhusu uchaguzi huo mnamo Alhamisi katika mkahawa wa Crowne Plaza jijini Nairobi, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki anayeongoza wachunguzi wa AU kwenye shughuli hiyo ametaja amani iliyoshamiri kote nchini kama jambo la kupigiwa mfano.

"Tulizuru takriban vituo 464 vya kupigia kura tangu vifunguliwe hadi shughuli ya upigaji ikaanza na kuisha, kuhesabu na kutuma kielektroniki ikakamilika. Mbali na Nyali Mombasa ambako maafisa wa usalama walilazimika kutuliza mzozo, sehemu zingine kote nchini usalama ulikuwa wa hali ya juu," akasema Bw Mbeki.

Zaidi ya maafisa 180,000 wa usalama walitumwa kote nchini kuimarisha usalama.

Aidha Rais huyu wa pili wa Afrika Kusini amepongeza tume ya IEBC na serikali kwa kushirikisha wahabusu katika jela kuonyesha demokrasia yao kwa kupiga kura.

"Tulizuru magereza na kushuhudia jinsi walivyopiga kura," akaeleza.

"Hakukuwa na shida zozote za kufunga vituo muda ulipowadia kwa mujibu wa sheria za IEBC. Vilifungwa kulingana na muda vilivyofunguliwa. Waliokuwa kwenye foleni wakati ulipofika, waliruhusiwa kushiriki uchaguzi," akaeleza.

Amesema kuwa maajenti wa IEBC na mawakala wa vyama vilivyoshiriki uchaguzi walishuhudia kila hatua ya shughuli hiyo.

"Mawakala walikagua kikamilifu kura zilizopigwa, zikahesabiwa wakiwepo, zikajazwa katika fomu 34A, wakatia sahihi na kurusu matokeo yatumwe kieletroniki," akaeleza Mbeki.

Hata hivyo mchunguzi huyu amesema ni mapema kutoa ripoti kamilifu kuhusu uchaguzi huo kwa sababu shughuli ya kuhesabu kura na kutangaza mshindi haijakamilika.

"Bado ni mapema kutoa ripoti kamili kwa sababu shughuli ya uchaguzi inaendelea. Japo amani iliyokuwepo siku ya uchaguzi ni ya kutia moyo. IEBC iliendesha uchaguzi huo na kuafikia matakwa ya AU na Wakenya," akadokeza Mbeki.

Muungano wa National Super Alliance (Nasa) kupitia kinara wake Raila Odinga unapinga matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kuhesabiwa, kujumuishwa katika kituo kikuu cha kuhesabu kura kilichoko Bomas of Kenya jijini Nairobi.

Kwa sasa Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee yuko kipau mbele kwa kura 8,075,296 uku Bw Raila akiwa na kura 6,668,886.

Nasa inasema matokeo hayo si halisi ikihoji kuwa mashine za IEBC zilidukuliwa na ndio maana Rais Kenyatta yuko mbele akisema yeye ndiye anaongoza.

"Kinara wa Nasa na vinara wenza walija kwetu, wakatueleza walipata habari hizo kupitia IEBC. Tuliwaeleza tutafanya uchunguzi, ifahamike vyema kazi yetu ni kuchunguza uhalisia wa uchaguzi, bali si kuchunguza mashine za tume. Hata hivyo tulichunguza kila hatua ya upigaji kura, hadi kutuma matokeo kieletroniki na ninaeleza wazi shughuli hiyo ilikuwa ya uwazi," akaeleza.

Akaongeza: "Kwa mfano mtu akiuawa, nitaeleza maafisa wa polisi waendeshe uchunguzi. Hata polisi mwenyewe akishuhudia mauaji yoyote, kortini hatasema aliona mauaji hayo, sharti kuwepo na uchunguzi. Ripoti yetu tutatoa baada ya miezi miwili na serikali ya Kenya ikituruhusu tufanye uchunguzi hatutasita kuuendesha."

Bw Mbeki aidha ameomba Wakenya na vinara waliohusika kwenhe uchaguzi kudumisha amani.

"Wakenya walifanya jambo la busara kuonyesha demokrasia yao kwa kushiriki uchaguzi. Hatutaki chochote kibaya kitendeke kwa mwananchi yeyote," akasema.