Ukungu watatiza safari za ndege JKIA

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  11:51

Kwa Muhtasari

Shughuli za usafiri wa ndege katika uwanja wa kimataifa wa JKIA jijini Nairobi mapema Ijumaa zimesitishwa kwa muda kutokana na ukungu unaoshuhudiwa.

 

NAIROBI, Kenya

SHUGHULI za usafiri wa ndege katika uwanja wa kimataifa wa JKIA jijini Nairobi mapema Ijumaa zimesitishwa kwa muda kutokana na ukungu unaoshuhudiwa.

Mamlaka ya huduma za ndege nchini (KAA) imetoa ripoti hiyo ikisema shughuli za ndege kutua na kupaa zitacheleweshwa, huku huduma hizo zikielezwa katika nyanja zingine kwa ajili ya ukungu.

"Kwa sababu ya ukungu mzito unaoshuhudiwa jijini Nairobi, shughuli za ndege kupaa na kutua zitacheleweshwa, zitaelekezwa katika nyanja zingine. Tunaomba wateja wawasiliane na kituo cha ndege kinachowahudumia kwa maelezo zaidi," KAA imechapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mamlaka hiyo pia imesema hali ya anga imeathiri huduma za ndege katika uwanja wa Wilson Airport.

Agosti 2, shirika la ndege la Kenya Airways lililazimika kuelekeza ndege zake zinazotua na kupaa katika viwanja vya ndege vinginevyo.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa awali ilisema hadi Agosti 13 Nairobi itashuhudia baridi, ukungu na mawingu hasa kila asubuhi.