http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885722/medRes/2191608/-/jaox6tz/-/swa.jpg

 

Mradi wa Sh10bn wa unyunyuziaji maji mashamba wa Lower Nzoia waanza Budalang'i

Mradi

Bango la mradi wa unyunyuziaji maji mashamba; Bunyala Irrigation Scheme. Picha/GAITANO PESSA 

Na GAITANO PESSA

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  10:19

Kwa Muhtasari

Mradi huo unalenga kufaidi kaunti za Busia na Siaya na umegawanywa mara mbili. 

 

BUSIA, Kenya

FAMILIA zaidi ya 100 zilizosalimisha ardhi kwa ajili ya utekelezwaji wa mradi wa unyunyuziaji mashamba maji wa Lower Nzoia katika eneobunge la Budalang'i zina kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali kuanza mchakato wa kuwafidia waathirika.

Meneja wa mradi huo wa Sh10 bilioni, mhandisi Edwin Manyonge kutoka Bodi ya unyunyuziaji mashamba (NIB), amesema kuwa tayari Wizara ya Maji imepokea mgao wa Sh450 milioni kutoka Hazina Kuu zitakazoelekezwa kwa Tume ya Ardhi nchini (NLC) kufanikisha mpango huo kwa awamu tatu. 

“Bajeti yote ya kuwafidia wakazi ni Sh1.5 bilioni japo kwa sasa tumepokea Sh450m ambazo zimeelekezwa kwa NLC,” Bw Manyonge amesema Ijumaa baada ya kutembelea Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong mjini Busia.

Aidha, meneja huyo amefichua kuwa mkandarasi wa mradi huo – kampuni ya Kichina ya SynoHdro – tayari ameanza shughuli za kubadilisha mkondo wa maji wa mto Nzoia (River diversion), uimarishaji wa kingo za mto huo (dykes) na vilevile sehemu ya kuingiza maji katika maeneo ya unyunyuziaji mashamba.

Mradi huo ambao unalenga kufaidi kaunti za Busia na Siaya umegawanywa mara mbili. 

Sehemu ya kwanza ya mradi huu inahusisha mikakati ya kukabiliana na mafuriko kupitia ujenzi wa kingo kando kando mwa mto Nzoia kwa kima cha Sh 1.4 b huku sehemu ya pili ikiwa ukukarabati wa unyunyizaji mashamba maji kwa kima Sh3.8 b. 

Zaidi ya ekari 4,000 zinatarajiwa kutumika katika mradi huo huku zaidi ya 34km ya kingo hizo zikikarabatiwa. 

Mradi wote unalenga kuhakikisha zaidi ya ekari 62,500 zinawekwa chini ya kilimo cha mpunga, mboga na matunda. 

Kwa mda mrefu mradi huo umekumbwa na upinzani si haba hasa kuhusiana na fidia, hatua ambayo ilichelewesha kuanzishwa kwake hata zaidi. 

Kusambaratisha mradi

Mwezi Oktoba, makundi ya kijamii – Bucodev na Bunyala Development Forum yalisisitiza kusambaratisha mradi huo iwapo swala tata la kuwapa wakazi hati miliki halitatatuliwa.

Akizunguza katika kikao cha uhamsisho wa wakazi, mshirikishi wa shirika la Bucodev Bw Tom Mango aliwataka wasimamizi wa mradi huo, bodi ya unyunyuziaji mashamba maji (NIB) kuangazia kwa uwazi swala hilo kabla ya mradi kuanzishwa rasmi. 

Alionya kuwa atawaongoza wakazi kupinga mradi huo iwapo hawatafidiwa kabla ya kuanzishwa kwake.