Usajili mpya wa watu kuanza nchini Kenya

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  10:56

Kwa Muhtasari

Ni utaratibu mpya ambao umepata umaarufu tangu litokee shambulio la Dusit Januari 15, 2019, jijini Nairobi.

 

NAIROBI, Kenya

SHUGHULI ya kusajili watu nchini inatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho alisema Alhamisi shughuli hiyo itaanza katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Januari 2019 hasa baada ya shambulizi la kigaidi katika hoteli ya Dusit jijini Nairobi lililosababisha vifo vya watu 21 wasio na hatia, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa lazima maelezo ya kila raia nchini yasajiliwe kwa mtambo wa kisasa wa Nimis.

Rais alisema mpango huu utasaidia serikali kukabiliana na visa vya uhalifu na kigaidi, ambapo idara ya usalama itaweza kufuatilia hali ya kila mwananchi mkasa unapotukia. Pia alisema shughuli hii itafanikisha mipango ya serikali katika utekelezaji wa maendeleo. 

Dkt Kibicho kwenye kikao na waandishi wa habari jijini Nairobi, alisema fomu maalumu yenye maswali yanayohusu mtu binafsi itajazwa. Aidha, hatua ya kwanza itakuwa kutambua uraia wa mtu.

"Tutahitaji vyeti kama kitambulisho cha kitaifa, cha kuzaliwa, NHIF, na nambari za KRA," alisema Dkt Kibicho.

Hati za usafiri

Alisema raia wa kigeni watahitajika kudokeza nchi wanayotoka na kuwasilisha pasi ya usafiri.

"Tutakagua iwapo wameoa (wanaume) au kuoleka (wanawake) na ikiwa wana kibali cha kufanya kazi nchini Kenya," alisema Bw Kibicho.

Shughuli hii pia itajumuisha kujua wazazi, na ikiwa mmoja hana wazazi wanaomtunza, alikozaliwa anayetoa maelezo na ulemavu. Fomu itakayojazwa ina nafasi ya kiwango cha elimu mtu alichohitimu, ajira; kuajiriwa au kujiajiri.

Dkt Kibicho alisisitiza kwamba chapa ya viganja vya mikono itachukuliwa, pamoja na ya viungo kadha vya mwili kama maskio na macho.