http://www.swahilihub.com/image/view/-/2963754/medRes/1181628/-/cjffrvz/-/maggie.jpg

 

Margaret Kenyatta: Utangamano ni muhimu kwetu Wakenya

Margaret Kenyatta

Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta ahutubu wakati wa ufunguzi wa Kampeni ya Kupunguza kwa Kasi Vifo vinavyohusiana na ubebaji Mimba barani Afrika (CARMMA) katika hoteli ya Intercontinental, Nairobi Novemba 19, 2015. Picha/PSCU  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  12:53

Kwa Muhtasari

Mama wa Taifa, mkewe Rais Uhuru Kenyatta, Bi Margaret Kenyatta, Jumatano aliwataka wenyeji katika Kaunti ya Wajir kudumisha amani.

 

MAMA wa Taifa, mkewe Rais Uhuru Kenyatta, Bi Margaret Kenyatta, Jumatano aliwataka wenyeji katika Kaunti ya Wajir kudumisha amani.

Bi Kenyatta aidha aliwarai wakazi wa kaunti hiyo na majirani zao kuhakikisha wamedumisha amani kabla, wakati na baada ya marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26.

"Ninawaomba muwe na uaminifu kwa familia zenu na taifa kwa ujumla kwa kudumisha amani," akasema Bi Kenyatta.

"Ninawasihi tuishi kwa utangamano, upendo na kusiwe na umwagikaji wa damu kama tulivyoshuhudia mwaka wa 2007/2008. Uchaguzi huja na kuisha, lakini nchi hii itasalia ilivyo," akaongeza.

Itakumbukwa kwamba ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007 zilisababisha vifo vya takriban watu 1,300 na maelfu kufurushwa kutoka makwao, wakawa wakimbizi wa ndani kwa ndani.

Kampeni

Hata hivyo Bi Kenyatta hakukosa kumpigia debe mumewe akisifu serikali yake kwa miradi ya maendeleo aliyofanya maeneo hayo, ikiwamo usambazaji wa stima kwa jamii zinazoishi huko na ujenzi wa barabara.

"Ninawasihi kama mlivyomchagua Rais Uhuru Kenyatta Agosti 8, mumpe kura kwa wingi zaidi wakati huu. Amejitolea kuimarisha maisha yenu, ninawahakikishia ataendelea kuwafanyia miradi mingi," akasema akiuza sera za Jubilee, ikiwa ni pamoja na huduma za uzazi bila malipo.

Ushindi wa Rais Kenyatta katika uchaguzi uliopita ulibatilishwa na mahakama ya juu, muungano wa Nasa ulipoupinga kwa madai kuwa ulikumbwa na udanganyifu.

Bi Kenyatta anafahamika kwa kampeni na miradi yake ya kuimarisha sekta ya afya.

Aidha Mama huyu hushiriki hafla za michezo kitaifa na hata kimataifa ili kuchangisha fedha za kufadhili sekta ya afya.