Vijana washauriwa kupata mafunzo ya uchimbaji madini

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  14:13

Kwa Muhtasari

Serikali ya Kaunti ya Kwale na Base Titanium imeshauri vijana kusomea kozi zinazoambatana na uchimbaji madini na ujenzi kwa lengo la kupata nafasi za kazi.

 

KWALE, Kenya

VIJANA wameshauriwa kusomea kozi zinazoambatana na uchimbaji madini na ujenzi kwa lengo la kupata nafasi za kazi.

Walishauriwa hayo na Serikali ya Kaunti ya Kwale na Base Titanium wakati wa kufuzu kwa vijana 32 wa shule za upili waliokuwa wakifanya kozi fupi katika kampuni ya Base Titanium.

Vijana hao walikuwa humo kwa siku 30 kusoma kutoka kwa wataalam wa migodi ili kuelewa vyema zaidi sekta hiyo.

Walifunzwa usalama, utoaji wa huduma ya kwanza na kuzima moto, uongozi, kushauriwa na jinsi ya kutumia kompyuta (ICDL).

Bw Mangale Chiporomondo, afisa mkuu wa elimu katika Kaunti ya Kwale wakati wa hafla hiyo alisema, “Serikali inapongeza Base Titanium kwa kufadhili mafunzo hayo kwa sababu inatusaidia kuhakikisha kuwa vijana wana ujuzi unaohitajika kupata kazi.”

Meneja wa Mafunzo Base Titanium Hamza Awadh alisema, “Ujuzi unaohitajika kuendesha sekta ya uchimbaji wa madini ni wa kiufundi, sio lazima iwe digrii,” alisema na kuongeza kuwa lengo kuu la kutoa mafunzo hayo ni kuchangia katika maazimio ya kitaifa.

Aliwashauri vijana kupata mafunzo ya kiufundi wakimaliza shule na kuongeza kuwa sekta ya kiufundi ina nafasi nyingi zaidi za kazi.