Vijana wazinduliwa

Na PETER ELIAS, Mwananchi

Imepakiwa - Tuesday, January 29  2019 at  11:56

Kwa Muhtasari

Vijana waanza kujengwa kiakili namna ya kujiajiri.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

TAASISI ya Ujasiriamali na Ushindani Tanzania (TECC) imewakaribisha wadau mbalimbali hasa Serikali na kampuni binafsi kushirikiana kutatua tatizo la ajira kwa vijana.

TECC ambayo inatoa mafunzo kwa vijana, kuwatafutia walezi wa biashara na kuwawezesha kupata mikopo, imebaini kuwapo kwa changamoto kubwa ya ajira nchini kwa vijana wasio na elimu na waliomaliza vyuo vya elimu ya juu.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TECC, Daniel Mghwira alisema taasisi hiyo inatoa mafunzo kwa vijana 90 kila mkoa katika mikoa minne ya Mtwara, Dar es Salaam, Pwani na Dodoma ambako wanatekeleza mradi wao wa “Jiandalie Ajira”.

“Tunatafuta wadau hasa Serikali ili tushirikiane nao kumaliza tatizo la ajira, peke yetu hatuwezi. Tunahitaji nguvu ili tuweze kuwafikia vijana wengi zaidi ambao wanahitaji mafunzo yetu,” alisema Mghwira.

Mghwira alisema katika utekelezaji wa majukumu yao, wamebaini kwamba ari ya kupenda ujasiriamali nchini imeongezeka kwa sababu sasa kuna uhitaji mkubwa wa mafunzo hayo kwa vijana waishio mikoa mbalimbali.

Mkurugenzi huyo alisema anaamini kwamba miaka 20 ijayo Tanzania itakuwa na wawekezaji wazawa wakubwa ambao watabadilisha mitazamo na maisha ya jamii ambayo haijali ujasiriamali kama fursa muhimu.

“Kwa ukubwa wa tatizo la ajira tuliouona na uhitaji wa vijana wa mafunzo haya, tumebaini kwamba mafunzo haya ya ujasiriamali yalitakiwa kutolewa miaka 20 iliyopita. Tunahitaji wadau wengine ili tufikie vijana wengi zaidi,” alisema Mghwira.

Ufikiaji hamasa

Naye meneja wa ufikiaji na hamasa, Abdul Juma alisema suala la ujasiriamali limekuwa halithaminiwi kuanzia kwenye ngazi ya familia, jambo linalosababisha vijana wengi kudai hawana ajira lakini wakiwa na fursa za ujasiriamali.

Juma aliitaka Serikali kuingiza suala la ujasiriamali kwenye mitalaa ya shule za msingi ili wakue wakiujua na kuupenda badala ya kupenda kuajiriwa na kulipwa mshahara mwisho wa mwezi.

“Ukiangalia familia zetu, zinamthamini mtu ambaye anafanya kazi benki na kutomthamini anayefuga kuku. Lakini ukiwaangalia vizuri, mfuga kuku ana kipato kikubwa,” alisema.