http://www.swahilihub.com/image/view/-/2942824/medRes/1166994/-/4j89ql/-/panyako.jpg

 

KNUN: Vitisho vya magavana havitamaliza mgomo

Seth Panyako

Mwenyekiti wa Muungano wa Wauguzi nchini (KNUN) Bw Seth Panyako (kati) akihutubia wanahabari jijini Nairobi. Picha/LEONARD ONYANGO 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, September 13  2017 at  11:17

Kwa Mukhtasari

Muungano wa wauguzi nchini (KNUN) umeshikilia hautasitisha mgomo wa wauguzi hadi pale matakwa yao yatakapotimizwa.

 

MUUNGANO wa wauguzi nchini (KNUN) umeshikilia hautasitisha mgomo wa wauguzi hadi pale matakwa yao yatakapotimizwa.

Aidha umeshikilia kuwa vitisho vya magavana kuwapiga kalamu na kuajiri wengine havitawababaisha.

"Sisi hatutatikiswa na vitisho vya magavana kufuta kazi wauguzi wanaogoma na kuajiri wengine," alisema Katibu Mkuu wa KNUN Bw Seth Panyako, akihutubia waandishi wa habari Jumanne jijini Nairobi.

Mwanzoni mwa wiki hii magavana walikuwa wametishia kufuta wauguzi wanaogoma kazi na kuajiri wengine.

Kulingana na KNUN ni kwamba mgomo wa wauguzi utasitishwa pale mkataba wao wa CBA utakapotiwa sahihi.

Juhudi za Baraza la Magavana (CoG) kujadiliana na KNUN kusitisha mgomo huo hata kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 hazikuonekana kuzaa matunda.

Hata hivyo Bw Panyako anasema endapo mazungumzo waliyokuwa nayo na magavana yangeendelea, huenda mgomo huo ungefikia kikomo.

"Sidhani iwapo vitisho vya magavana vitafanya turejee kazini ikikumbukwa jinsi tumepitia madhila chini yao. Mkataba wa CBA uliotiwa sahihi ndio utafanya turudi kazini, la sivyo tutaendelea kuweka zana zetu za kazi chini," akasema Katibu huyo.

Gavana wa Turkana Josphat Nanok ndiye mwenyekiti wa CoG.

Tume ya kuainisha na kudhibiti mishahara ya watumishi wa umma (SRC) awali ilifichua matakwa wanayotaka yatekelezwe wauguzi ni ghali mno na yatapelekea mlipa ushuru kugharamika zaidi.

KNUN ilidinda kuafikiana na tume ya SRC inayoongozwa na mwenyekiti wake Bi Sarah Serem.

Wizara ya Afya chini ya Waziri wake Dkt Cleopha Mailu pia imeonekana kushindwa kuafikia dayalojia na KNUN.

Mgomo huo, Jumatatu uliingia siku yake ya 100 huku Wakenya wanaohitaji huduma za wauguzi wakitaabika.