http://www.swahilihub.com/image/view/-/4961684/medRes/2239664/-/q4t2mjz/-/ikoniki.jpg

 

Vuguvugu la kupambana na ufisadi labuni mikakati ya kufanikisha kazi hiyo

Dkt Wilfred Kiboro

Dkt Wilfred Kiboro ambaye ni mwanachama wa Bodi ya Shirika la Habari la Nation (NMG) ahutubu akiwa na wanachama wengine wa kamati inayoongoza juhudi mpya za kupambana na ufisadi (Multi-Sectoral Initiative Against Corruption -MSIAC) Januari 31, 2019, jijini Nairobi. Picha/CHARLES WASONGA 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  13:50

Kwa Muhtasari

Kamati inayoongoza juhudi mpya za kupambana na ufisadi (Multi-Sectoral Initiative Against Corruption -MSIAC) inasema kuundwa kwa kamati za nidhamu katika miungano yote ya kitaaluma zenye mamlaka ya kufutilia mbali leseni za wanachama watakaohusishwa na ufisadi ni njia mojawapo ya kukabiliana na ufisadi.

 

NAIROBI, Kenya

KAMATI inayoongoza juhudi mpya za kupambana na ufisadi (Multi-Sectoral Initiative Against Corruption -MSIAC) imebuni mikakati inayolenga kufanikisha vita dhidi ya ufisadi nchini.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuundwa kwa kamati za nidhamu katika miungano yote ya kitaaluma zenye mamlaka ya kufutilia mbali leseni za wanachama watakaohusishwa na ufisadi.

Mwenyekiti wa Baraza la Miungano ya Mashirika ya Kitaaluma Afrika Mashariki (Council of Association of Professional Societies in East Africa) Bi Irene Wanyoike Alhamisi alisema kuwa baadhi ya mashirika wanachama wa baraza hilo tayari yameanza kuwaadhibu wanachama wao waliopotoka kimaadili kama ishara ya kuonyesha kujitolea kwao katika vita dhidi ya ufisadi.

"Kwa mfano, tayari Bodi ya Kuwasajili Wasanifu Majengo na Masoroveya (Board of Registration od Architects and Quantity Surveyors) imeanza kufutulia mbali usajili wa wanachama wao waliopatikana na doa la ufisadi. Leseni zao za kuhudumu pia zimetwaliwa," akasema Bi Wanyoike.

"Vilevile, tumekuwa tukishuhudia Chama cha Mawakili Nchini (LSK) iliwaondoa mawakili wafisadi kwenye orodha ya mawakili huku Taasisi ya Wataalamu ya Uwekezaji  na Wachanganuzi wa Masuala ya Kifedha (Institute of certified Investment and Financial Analysts juzi ikichapisha orodha ya wanachama wake ambao maadili yao ni ya kutiliwa shaka," Bi Wanyoike akaongeza.

Kuzingatia kanuni

Naye Dkt Wilfred Kiboro, ambaye ni mwanachama wa Bodi ya Shirika la Habari la Nation (NMG) alisema sekta ya uanahabari imepiga hatua katika vita dhidi ya ufisadi kwa kuhakikisha kuwa wadau katika sekta hiyo wanazingatia kanuni za taaluma hiyo.

"Kwa kushirikiana na Baraza la Vyomba vya Habari Nchini (MCK) tumehakikisha kuwa kanuni hizi zinatekelewa kwa kuwachakulia hatua wanahabari bandia na wafisadi ambao lengo lao ni kuharibu sifa ya taaluma hii," akasema alipojumuika na wanachama wengine kwenye kikao na wanahabari katika hoteli ya Intercontinental Nairobi.

Hata hivyo, alitoa wito kwa wanahabari kuendeleza juhudi ya kuangazia stori zinazofichua kashfa za ufisadi katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

“Vyombo vya habari vimefanya kazi nzuri kuwa kuhakikisha uwajibikaji katika matawi yote matatu ya serikali kwa kufichua kashfa za ufisadi miongoni mwa maafisa wa umma. Kurunzi ya wanahabari pia inapasa kuelekezwa katika serikali za kaunti ambazo pia zimeathiriwa na uozo wa ufisadi,” akasema Bw Kiboro.

Alisema inasikitisha kuwa gharama ya kuweka lami kilomita moja ya barabara imepanda hadi kufikia Sh30 milioni badala ya Sh22 milioni kwa sababu magavana huwalazimisha wakandarasi kuwapa kima cha Sh6 milioni kwa kila kilomita ya barabara ya lami wanayojenga.

“Nyie kama wanahabari mwapaswa kufichua sakata kama hizo kama njia ya kuwaaibisha viongozi kama hao,” Bw Kiboro akasisitiza.

Asikitika

Alisema inasikitisha kuwa japo wanahabari wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kuwajuza wananchi kuhusu mienendo mibaya ya viongozi, hasa wanasiasa, wamekuwa wakilaumiwa bila sababu yoyote.

“Kwa mfano tukiripoti kuwa wabunge huketi mikahawani wakifurahia mlo na vinywaji murwa badala ya kuhudhuria vikao kujadili masuala yenye umuhimu kwa umma huku wajifurika bungeni hoja ya kujiongezea mapato inapojadiliwa tunalaumiwa kwa kusema ukweli huu,” Bw Kiboro akaongeza.

Mwenyekiti wa kamati simamizi ya mpango huo Bw Lee Karuri alisema kuwa mikakati iliyoratibiwa na kundi hilo inatokotana na kongamano kuhusu ufisadi ambao ulifanyika wiki jana katika ukumbi wa Bomas of Kenya Nairobi wiki jana.

Alisema kamati yake itafuatilia kwa karibu kuhakikisha kuwa ahadi ambazo wakuu wa vitengo vyote vya serikali kuu, Afisi Kuu, Bunge na Idara ya Mahakama, vilitoa katika kongamano hilo vinatimizwa.

“Tutafuatilia kwa karibu kuhakikisha kuwa yale yaliyofikiwa Bomas hayasalii ahadi zisizotimizwa. Hilo halikuwa jukwaa la watu kulaumiana bali kuhimiza uwajibikaji kutoka kwa matawi yote ya serikali na asasi zinazohusika katika vita dhidi ya ufisadi,” akasema Bw Karuri.