http://www.swahilihub.com/image/view/-/4741310/medRes/2097975/-/mcndvez/-/mfumk.jpg

 

VAT: Vuguvugu lalitaka bunge kutupilia mbali pendekezo la Rais Kenyatta

Michael Kang'ethe

Bw Michael Kang'ethe, mhudumu wa tuktuk Githurai 45, Kiambu ambapo nauli ya usafiri kupitia magari hayo imeongezeka mapema Jumatatu, Septemba 3, 2018 kufuatia ongezeko la bei ya mafuta nchini baada ya kutozwa VAT ya asilimia 16. Picha/SAMMY WAWERU 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  20:19

Kwa Muhtasari

Kundi la African Human Rights Outreach Initiative (AHROI) limesema Rais Uhuru Kenyatta alifaa kufuata mswada wa bunge la kitaifa uliopitishwa hivi majuzi na unaotaka ushuru wa VAT kwa bidhaa zote za petroli wa asilimia 16 ambao Ijumaa ulipunguzwa kwa asilimia nane, uahirishwe kwa miaka miwili hadi mwaka 2020.

 

VUGUVUGU la kutetea haki za binadamu limelitaka bunge la kitaifa nchini Kenya litupilie mbali pendekezo la Rais Uhuru Kenyatta la Ijumaa la kupunguza ushuru wa nyongeza kwa bidhaa za petroli kutoka asilimia 16 hadi asilimia nane.

Kundi hilo la African Human Rights Outreach Initiative (AHROI) limesema kuwa Rais alifaa kufuata mswada wa bunge hilo uliopitishwa hivi majuzi kuwa ushuru huo uahirishwe kwa miaka miwili hadi mwaka 2020.

Kundi hilo limeteta kuwa rais Kenyatta anafaa kushinikizwa na bunge hilo atekeleze sera za kiuchumi ambazo zinaambatana na pato la taifa bila kujiingiza kwa mikopo kiholela.

Baada ya rais kutangaza hayo Ijumaa alasiri, sasa bunge ambalo liko likizoni ya mwezi mmoja linahitajika kuitwa kwa hali ya dharura wiki ijayo na Spika Justin Muturi kujad0ili pendekezo hilo na ambapo liko huru kupitisha au kutupilia mbali maoni ya Rais.

Mwakilishi wa kikundi hicho katika kanda ya Kati na Kaskazini mwa Kenya Bw Robert Muraguri alisema kuwa Rais Kenyatta na serikali yake anafaa kugundua kuwa nyongeza ya ushuru bila nyongeza ya pato kwa wanaotegemewa kukatwa ushuru huo ni hesabu ya ukandamizaji kiuchumi.

"Anafaa ajiulize ni lipi aliongeza wafanyakazi mishahara kwa kiwango cha asilimia 16 au asilimia nane. Anafaa ajiulize kama kuna ushahidi kuwa utajiri wa Wakenya hasa wa kiwango cha chini umeongezeka kwa asilimia hiyo ya nyongeza ya ushuru; na jibu ni la," Muraguri ameelezea Swahili Hub.

Adinda kutia saini

Rais Kenyatta baada ya kupokezwa mswada huo wa bunge kuhusu kuahirisha utekelezaji wa nyongeza hiyo ya ushuru alikataa kuuweka sahihi uwe sheria na badala yake akaurejesha bungeni ili ufanyiwe maerekebisho ya kutekelezwa ili iwe ni sasa japo kwa shoka hilo la asilimia 50.

Ikiwa bunge litakubaliana naye, gharama ya maisha inatarajiwa kuongezeka bado kwa asilimia nane kwenda juu ikilinganishwa na hali ya awali ya mfumko wa kuanzia asilimia 16 kwenda juu.

Bw Muraguri aliteta kuwa wito wa rais kwa wafanyabiashara wa bidhaa na huduma hapa nchini wateremshe bei zao kwa Wakenya ni sawa na kuongea kna mawe jangwani "kwa kuwa mfumo wa biashara duniani ni huru ambapo unaweza ukaweka bei ya bidhaa zako na huduma pia kwa kiwango utakavyo bora tu uwachumbie wateja wanunue."

Alisema mfumo huo wa biashara huru ni hatari kwa kuwa walio na pesa huwa hawabishani na huteka nyara soko huku mlala hoi akibakia bila afueni na anaweza akalala njaa kwa kuwa unga wote madukani ulinunuliwa na walio na chao.

Vuguvugu hili ndilo lilikuwa limefadhili mashtaka dhidi ya serikali baada ya kutangaza nia ya kutekeleza nyongeza hiyo ya Ushuru Septemba Mosi.

Bw Muraguri alisema kuwa kipengele cha 43 cha katiba mpya kiko wazi kuwa kila Mkenya ako na haki ya kupata afya, usafi, chakula, elimu, maji safi na usalama wa kijamii kwa wakati wowote ule, hali ambayo alisema imedunishwa kuwa ya ugumu zaidi katika nyongeza hiyo ya ushuru wa mafuta.

"Nacho kipengele cha 22 kinatoa mwanya wa kila mtu kwenda mahakamani kushtaki serikali kwa kukiuka haki hizo za kimsingi bila kufuata utaratibu wa mahakama na pia bila malipo yoyote," akasema.

Aidha, alisema kuwa katika vigezo vya umoja wa Mataifa (UN) kuhusu haki za  binadamu, wananchi katika taifa ambalo halina uwezo wa kulisha wananchi wake hujumuishwa katika fani ya mataifa ambayo yamefeli.

Alisema kuwa uongozi hutekelezewa binadamu na mali zao na ni lazima wananchi hao kwanza wapate maisha bora kabla ya kuandaliwa mikakati mingine yoyote ya kimaendeleo, hivyo basi kudunisha tetesi za rais kuwa taifa linahitaji mikopo ili liandae miradi ya maendeleo.

"Itakuwaje umvishe Mkenya vazi la ugumu wa maisha ukimwandaa kumvisha vazi la kujengewa barabara? Ni lipi la dharura katika maisha ya binadamu: Ni lishe, afya na makao au ni ujenzi wa barabara ambazo tunaambiwa ndizo zinafanya serikali kukopa kiholela na kisha kuwatoza Wakenya ushuru kwa njia za kikatili ili walipie mikopo hiyo?" akahoji.