http://www.swahilihub.com/image/view/-/2412312/medRes/804970/-/10ai54jz/-/dnMurang%2527agovernor3108.jpg

 

Mwangi wa Iria alia kuhusu genge la kisiasa Murang'a

Mwangi wa Iria

Gavana wa Murang'a Mwangi wa Iria akihutubia wanahabari awali. Picha/JOSEPH KANYI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  15:02

Kwa Mukhtasari

Gavana wa Murang’a Bw Mwangi wa Iria Jumatano amemtaka kamishna wa Kaunti hiyo Bw John Elungata achunguze kwa dharura genge la kisiasa katika Kaunti hiyo analodai lina msingi sawa na lile la Mungiki.

 

GAVANA wa Murang’a Bw Mwangi wa Iria Jumatano amemtaka kamishna wa Kaunti hiyo Bw John Elungata achunguze kwa dharura genge la kisiasa katika Kaunti hiyo analodai lina msingi sawa na lile la Mungiki.

Akiongea mjini Murang’a, Wa Iria amesema kuwa amewasilisha habari muhimu kwa Bw Elung’ata na “ni juu yake sasa atekeleze alilopewa kama jukumu moja baadhi ya zingine katika ajira yake ya kuweka watu salama.”

"Nimempa (Elungata) habari kuwa genge hilo linafahamika kama “Nja Nene (Boma Kubwa) na ambalo limeundwa na mwanasiasa mmoja wa Kaunti hii,” amesema gavana Wa Iria.

Bila kutaja jina la mwanasiasa huyo, Wa Iria alisema kuwa wafuasi wa kundi hilo wamekuwa wakirandaranda mitaani wakitoa vitisho kwa raia na kuwashinikiza wapige kura zao kwa mwanasiasa fulani la sivyo watakipata cha mtema kuni baadaye.

Wa Iria aliteta kuwa “ni hivi majuzi tu katika mji wa Kenol ambapo wafuasi wa genge hilo wakiandamana na mwanasiasa anayewafadhili walizua patashika huku wakiwa na jezi rasmi za ugenge wao na jina la mwanasiasa huyo likiwa limeandikwa kwa jezi hizo.”

Alisema kuwa genge hilo ndilo hutoza wahudumu wa matatu ada haramu katika barabara ya Kaharate kuelekea Kigumo “na hadi sasa maafisa wa polisi licha ya kuwa na ufahamu huo, hawajafanya lolote kulithibiti.”

Kuvunja

Bw Wa Iria alisema kuwa hadi sasa maafisa wa kiusalama wa Kaunti ya Murang’a wako na habari kuhusu genge hilo na mfadhili wake, lakini “kwa sababu ambazo lazima watuelezee, hawaoni la dharura kulivunja.”

Mshirikishi wa masuala ya kiusalama katika eneo la Kati Bw Naftaly Mung’athia amethibitishia Swahilihub kuwa kamati ya eneo kuhusu usalama iko na habari hizo.

“Sio tu katika Kaunti ya Murang’a. Tuko na habari muhimu kuhusu magenge ya kisiasa kutoka Kaunti za Nyeri, Kirinyaga, Kiambu na Nyandarua. Tunaweka mikakati ya kuvunja magenge hayo yote. Namtaka Bw wa Iria atulie na atupe nafasi. Tutaingia huko kwake na genge hilo litaona mwisho wa mwangaza,” akasema.