Wanne waaga dunia wakisherehekea ushindi wa Rais Kenyatta

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, August 12  2017 at  12:02

Kwa Mukhtasari

Wafuasi wanne wa mrengo wa Jubilee kisiasa wameripotiwa kuaga dunia katika Kaunti ya Nakuru baada ya kugongwa na gari wakiwa barabarani kusherehekea ushindi wa Rais Kenyatta wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

 

WAFUASI wanne wa mrengo wa Jubilee kisiasa wameripotiwa kuaga dunia katika Kaunti ya Nakuru baada ya kugongwa na gari wakiwa barabarani
kusherehekea ushindi wa Rais Kenyatta wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Inadaiwa wanne hao walikuwa wamejitokeza katika eneo la Mai Mahiu lililoko katika Kaunti ndogo ya Naivasha na ambapo baada ya kushuhudia tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ikitangaza matokeo hayo kwa runinga, wakajitokeza nje kusherehekea.

Afisa msimamizi wa Askari Tawala eneo hilo, Kevin Opete amethibitisha kufariki kwa watu hao.

"Ndio tumekumbana na mkasa wa watu wanne kugongwa na gari na kuaga dunia wakiwa barabarani kusherehekea ushindi wa rais Kenyatta,” amesema Opete.

Ameambia mtandao wa Swahilihub kwa simu kuwa wanne hao walikuwa miongoni mwa wengine wengi ambao mwendo wa saa tano usiku walikuwa katika barabara ya lami eneo hilo wakiendelea na sherehe zao.

Opete amesema kuwa shida iliwakumba watu hao baada ya gari moja ndogo kuwapenya kwa kuwa lilikuwa kwa mwendo wa kasi na dereva hakuwa na
habari kuwa barabara ikiwa na umati huo.

“Gari hilo halikuwa na dereva aliyekuwa na nia ya kuua watu au kuwajeruhi. Hilo tunaelewa kutokana na utathimin wa hali. Ni watu hao walioingia barabarani na ambapo ni wazo hatari na lililo kinyume cha sheria. Mauti haya yangezuilika iwapo sherehe hizo zingekuwa za kuchukua tahadhari ya kiusalama,” akasema.

Hata hivyo, amesema kuwa dereva wa gari hilo alitiwa mbaroni pamoja na gari lake na maafisa wa kituo cha Mai Mahiu na ambapo baada ya
kuandikisha taaroifa ya habari, aliachiliwa huru.

“Ni utaratibu wa kushughulikia ajali za barabarani ambapo dereva na gari lake hutiwa mbaroni, dereva anaandikisha taarifa na kisha kuachiliwa na baadaye hali ya ajali hiyo inatathiminiwa na iwapo kuna mashtaka ambayo yataandaliwa dhidi yake, mikakati hiyo inafuata baadaye,” akasema.

Alionya wenyeji na pia wakenya wengine wachukue tahadhari na iwapo wangetaka kusherehekea barabarani, “wachukue tahadhari kuu ya kujiepusha na kutembea katika barabara za lami, wasifunge barabara na watekeleze maamuzi tu yale ya kuwaweka salama.”