http://www.swahilihub.com/image/view/-/2849078/thumbnail/1104176/-/4w28v1z/-/maanda.jpg

 

Maandamano yafanyika kuisuta serikali kuhusu Katiba

Maandamano

Kundi la "The Green Amendment Camp" lililobuniwa na Mbunge wa Ndhiwa Agostihno Neto na ambalo linaunga mkono kupitshwa kwa mswada wa kufanikisha usawa wa kijinsia kwa chini ya kanuni ya thuluthi ta, lafanya maandamano jijini Nairobi Agosti 27, 2015 kulalamikia hatua ya serikali kujikokota kutekeleza kikamilifu Katiba Mpya. Picha/CHARLES WASONGA  

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, August 27  2015 at  20:04

Kwa Muhtasari

Makundi na mashirika ya umma yalifanya maandamano katika barabara za jiji la Nairobi yakiisuta serikali kwa kuchelewesha utekelezaji wa Katiba, miaka mitano baada ya kuzunduliwa kwake.

 

MAKUNDI na mashirika ya umma Alhamisi yaliandamana katika barabara za jiji la Nairobi yakiisuta serikali kwa kuchelewesha utekelezaji wa Katiba, miaka mitano baada ya kuzunduliwa kwake.

Huku wakibeba mabango yenye maandishi ya "KATIBA DAY" wanaharakati hao kwanza walikongamana katika eneo la Freedom Corner katika bustani ya Uhuru Park, waliandamana katika barabara za Kenyatta Avenue, Kimathi street, Moi Avenue na Harambee Avenue hadi katika majengo ya bunge.

Vile vile waandamanaji hao waliwataka wabunge wapitishe mswada kuhusu usawa wa kijinsia,wakisema kutopitishwa kwa sheria hiyo kunawanyima akina mama haki yao ya kikatiba.

"Inasikitisha kuwa ingawa ni miaka mitano tangu Katiba hii mpya ianze kufanya kazi, wananchi hawajahisi manufaa yake kwani serikali imekuwa ikichelewesha miswada inayopasa kufanisha utekelezwaji wake," akasema mmoja wa waandamanaji hao, John Makumi.

Bw Makumi ambaye ni mwanachama wa kundi la kutetea haki za kibinadamu la Super Ethnic Minority Forum alitoa mfano wa kucheleweshwa kwa miswada 28 iliyonuiwa kufanisha vipengee muhimu vya katiba kama ishara kwamba serikali haina nia ya kufanisha utekelezaji wa katiba.

Kundi la "The Green Amendment Camp" pia lilishiriki katika maandamano hayo yaliyoanza saa nne asubuhi na kuendeshwa kwa amani.

Kundi hilo ambalo lilibuniwa na Mbunge wa Ndhiwa Agostihno Neto, limekuwa likiunga mkono kupitshwa kwa mswada wa kufanikisha usawa wa kijinsia kwa chini ya kanuni ya thuluthi tatu.

"Haki kwa Mama"

Huku wakibeba bango lenye maandishi, "Haki kwa Mama, Usawa kwa Jamii" waliwasuta wabunge kwa kuchelewesha kupitishwa kwa mswada huo.

Wengine walisikika wakimsuta mwenyekiti wa Tume ya Utekelezaji wa Katiba (CIC) Bw Nyachae kwa kile walichokitaka kama hatua yake ya "kuingiza siasa katika mchakato wa utekelezaji wa Katiba".

Wakati huo huo, shughuli za maadhimisho miaka mitano tangu kuzinduliwa kwa Katiba katika sehemu mbali mbali humu nchini huku CIC ikiandaa maadhimisho hayo katika uwanja wa michezo wa Kisii. Chama cha Cord nacho kiliandaa hafla kama hizo katika makao yake makuu, jumba la Orange House, Nairobi.