http://www.swahilihub.com/image/view/-/2936596/medRes/1162672/-/2c2bdn/-/DNCOASTSAVULA0908C.jpg

 

Wabunge wa ANC waunga mkono juhudi za Rais Kenyatta

Ayub Savula

Mbunge wa Lugari Ayub Savula akihutubuia wanahabari. Picha/KEVIN ODIT 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  13:29

Kwa Muhtasari

Alichokianzisha Moses Kuria kinazungumzwa kila kona ya taifa.

 

NAIROBI, Kenya

KAULI ya mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria iliyoonekana kuchamba Rais Uhuru Kenyatta kuwa amepuuza eneo la Mlima Kenya kimaendeleo, inaendelea kukosolewa na viongozi mbalimbali nchini.

Ijumaa wabunge wa Amani National Congress (ANC), chama kinachoongozwa na kinara mwenza wa Nasa, Musalia Mudavadi, wameyakashifu wakisema Rais si kiongozi wa jamii moja pekee ila ni wa taifa lote.

Wakihutubia waandishi wa habari jijini Nairobi, wabunge hao wamesema wanaunga mkono maridhiano ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuunganisha taifa, maarufu Handshake. Machi 9, 2018, viongozi hawa walitangaza kuweka kando tofauti zao za kisiasa za tangu jadi na kuahidi kuunganisha taifa, kupigana na ukabila, ufisadi na kufanyia wananchi maendeleo.

Wabunge wa ANC wamesema Rais Kenyatta hafai kubabaishwa na yeyote, na kwamba ashikilie msimamo wake wa kuhakikisha maendeleo yanatekelezwa katika kila kona ya taifa.

"Kwa hivyo viongozi wanaolalamika na kumkosea Rais heshima wajue yeye ni nembo la taifa, maendeleo yanapaswa kufanywa kila sehemu ya nchi," amesema Ayub Savula, mbunge wa Lugari.

Bw Savula ambaye ameongoza wabunge wenza ANC kueleza kauli ya chama hicho kuhusu matamshi ya Kuria, amesema kinaunga ajenda kuu nne za Rais Kenyatta ambazo ni; makazi bora na nafuu, afya kwa wote, ujenzi wa viwanda na usalama wa chakula.

Matamshi ya Kuria yaliungwa mkono na mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri.

Utengano

Kulingana na Tindi Mwale, ambaye ni mbunge wa Butere ni kwamba viongozi hao wanataka kuleta utengano wa taifa.

"Maendeleo hayatafanywa eneo la Kati pekee. Tunaunga mkono msimamo wa Rais, afanye kazi. Viongozi hao wanataka kutenganisha hii nchi. Kenya ni moja, afanye maendeleo Kenya nzima," amesema Bw Tindi.

Katika mkesha wa kuukaribisha mwaka wa 2019, Kuria alidai Rais Kenyatta ametelekeza eneo la Kati kimaendeleo, akiegemea maeneo ya upinzani na ambayo alisema hayakumchagua kwa wingi kama Mlima Kenya. Matamshi yake "hii mambo kazi yetu ni kupiga kura halafu maendeleo yanaenda kwingine, hii ujinga tuwache," yamekashifiwa vikali na viongozi kadha wa chama tawala cha Jubilee wakimtaka aheshimu Rais.

Rais Kenyatta ameshikilia kuwa atafanya maendeleo kote nchini.

Moses Kuria ameomba Rais msamaha, akionekana kujutia matamshi yake.