http://www.swahilihub.com/image/view/-/3141592/medRes/373394/-/fqrkgy/-/DNMilk0305b.jpg

 

Wafugaji katika sekta ya maziwa wataka bodi ya New KCC ivunjwe

Maziwa

Mkulima akama ng'ombe. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Monday, January 28  2019 at  07:50

Kwa Muhtasari

Baadhi ya wafugaji wa ng'ombe wa maziwa walalama New KCC imejisahau.

 

MURANG'A, Kenya

WAZALISHAJI maziwa hapa nchini wikendi walipendekeza bodi ya New KCC ivunjwe wakisema kuwa imepoteza ufahamu wa kazi yake.

Walisema kuwa bodi hiyo inahujumu kampuni hiyo kwa kutoa maelekezo duni ambayo hayaambatani na sera za kuikuza.

Aidha, walitishia kujiondoa kutoka kwa New KCC ikiwa haitaongeza bei inayotoa  kwao ambayo wiki mbili zilizopita iliangushwa kwa asilimia 15 kwa kisingizio kuwa kiwango cha uzalishaji kimezidisha maziwa nchini hivyo basi kushukisha bei katika soko.

Kutoka Sh35 ambazo kampuni hiyo ilikuwa ikitoa kwa lita moja ya maziwa, kwa sasa imetangaza bei ya Sh30.

Wakiongea Jumamosi katika mkutano uliofanyika katika Taasisi ya Kilimo ya Jomo Kenyatta Kaunti ya Murang'a, miungano inayounda Shirika la Mt Kenya Dairy Association likiongozwa na Katibu wake Bw Samuel Njogo, walisema kwa sasa bodi ya New KCC inashirikiana na wapinzani wa kibinafsi kuwanyanyasa.

Bodi hiyo ingefaa kujua wapinzani wake walikuwa wakinunua lita moja ya maziwa kwa Sh40 na kisha wakaiangusha hadi Sh35. Bei hiyo ingewagutusha washiriki wa bodi ya New KCC kutulia kwa bei yao ili kuimarisha usajili wa memba wapya," akasema Bw Njogo.

Bw Njogo alidai kuwa kuna ushirikiano mkuu kati ya baadhi ya wakurugenzi katika bodi hiyo na wale wa kampuni pinzani ambayo humilkiwa na watu tajika katika serikali.

"Kumekuwa na mikakati makusudi ya kuangusha New KCC ili kampuni hiyo ya kibinafsi ijipatie ukiritiba katika sekta ya maziwa. Bodi ya New KCC ndiyo inatumiwa kutekeleza njama hiyo," akasema.

Hata hivyo, akiongea kwa simu na mtandao wa Swahili Hub, Mwenyekiti wa Bodi ya New KCC Bw Matu Wamae alikana madai hayo akisema kuwa kuangushwa kwa bei hiyo kumetokana na ongezeko la maziwa.

"Tukipokea maziwa nyingi kupita kiasi huwa tunalazimika kuihifadhi kupitia uundaji wa bidhaa za muda mrefu sokoni. Soko la bidhaa hizo huwa ndogo kiasi kwamba hutupa shida za kifedha," akasema.

Alisema kwa sasa kiwango cha bidhaa hizo zimegonga lita 10,000 kwa siku, hali ambayo alisema lazima ikabiliwe na mikakati ya kuangusha bei ya ununuzi ili kuhifadhi pesa za utengenezaji wa maziwa ya ziada.