http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885646/medRes/2191563/-/cbihm0/-/hota.jpg

 

Wahitimu wa MKU wahimizwa kuwa wabunifu

Mount Kenya

Baadhi ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya waliofuzu Ijumaa, Desemba 7, 2018, katika chuo hicho mjini Thika. Picha/LAWRENCE ONGARO 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  14:47

Kwa Muhtasari

Wahitimu wanafaa kuwa wabunifu na ikiwezekana watumie ujuzi wao kubuni nafasi za ajira.

 

THIKA, Kenya

KUNA haja ya kujituma na kujitegemea baada ya kufuzu elimu ya chuo kikuu.

Mwenyekiti wa bodi ya Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) mjini Thika, Profesa Simon Gicharu, aliwahimiza wahitimu 4,500 waliofuzu kuwa cha muhimu ni "kutumia ujuzi wako kubuni ajira yako mwenyewe."

Amewahimiza wajifunze kutafuta kwa jasho badala ya kutamani vitu vinavyopatikana kwa urahisi ambavyo baadhi ni hatari mno.

"Vijana wengi siku hizi wanatamani mali ya kujileta haraka. Nawahimiza muwe na subira na kujifunza kutia bidii ili kupata huo utajiri," amesema Prof Gicharu.

Ameyasema hayo leo Ijumaa katika uwanja mkuu wa chuo hicho kilichoko eneo la Landless mjini Thika.

Amesema ni sharti mtu kuanza chini hadi kufika kileleni kwa njia za haki badala ya kukimbilia mambo kwa pupa na baadaye kuporomoka.

Ameiomba Wizara ya Vijana kufanya hima kuona ya kwamba vijana wanasaidiwa ili kujiendeleza kimaisha.

"Kwanza vijana wanaojiajiri katika mitandao ya kijamii kama Bloga wanastahili kupewa nafasi ya kujiendeleza zaidi badala ya kuachwa hivyo," amesema Prof Gicharu.

Hoteli ya kifahari

Amesema chuo cha Mount Kenya kinatarajia kufungua hoteli ya kifahari ambayo pia itakuwa muhimu kwa wanafunzi wa chuo hicho kufanyia mazoezi yao ya kielimu huko.

Mgeni wa heshima katika hafla hiyo, Profesa Chacha Nyaigoti Chacha ametilia msisitizo umuhimu wa kuzingatia ubunifu na maswala ya utafiti katika chuo hicho.

"Ili kupiga hatua katika masomo ya juu ni sharti vyuo vikuu kuzingatia utafiti na ubunifu. Dunia ya sasa inapiga hatua ya kiteknolojia na kwa hivyo ni vyema mambo pia kubadilika," amesema Prof Chacha.

Amewapongeza wahadhiri kwa kufanya kazi njema ya kuwanoa wahitimu hao hadi kiwango cha kupata shahada jambo alilotaja kama hatua kubwa.

Wakati wa hafla, hiyo wabunge wawili, Bw Charles 'Jaguar' Kanyi wa Starehe, na mwenzake Badi Twalib wa Njomvu wametuzwa shahada za digirii katika maswala ya kibiashara na mipango.

Wakati huo pia Chifu wa kutumia mitandao ya kijamii wa Lanet kaunti ya Nakuru, Bw Francis Kariuki, ametuzwa shahada ya uzamili katika saikolojia na ushauri nasaha.

Amesema amepiga hatua kubwa kielimu na kwa hivyo kazi yake ya kutumikia wananchi itakuwa rahisi kwake.

"Kama aliyejifunza saikolojia nitakuwa na nafasi nzuri ya kutatua shida nyingi za wananchi. Nimefurahi kufikia kiwango hicho," alisema Bw Kariuki.

Viongozi hawakuficha furaha yao kutokana na hatua kubwa waliopiga kielimu.

Walisema sasa watawatumikia wananchi kwa njia ya uwazi na uadilifu huku wakisema ni mwamko mpya kwa "sisi viongozi".