http://www.swahilihub.com/image/view/-/4955228/medRes/2235982/-/11nauofz/-/ukiak.jpg

 

Wakazi wa Budalang'i kupata hatimiliki kuwezesha utekelezwaji mradi wa Lower Nzoia

Gideon Mung'aro

Katibu msimamizi katika Wizara ya Ardhi Gideon Mung'aro (katikati) akizumgumza na wanahabari katika afisi za ardhi mjini Busia. Amesema wizara yake inaharakisha shughuli ya utoaji hatimiliki kwa wakazi wa Budalang'i ili kutoa nafasi kwa utekelezwaji wa mradi wa Sh10 bilioni wa unyunyizaji mashamba maji wa Lower Nzoia unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Picha/GAITANO PESSA 

Na GAITANO PESSA

Imepakiwa - Monday, January 28  2019 at  16:01

Kwa Muhtasari

Tayari hatimiliki 8,000 ziko tayari kutolewa, kulingana na katibu msimamizi katika Wizara ya Ardhi Gideon Mung'aro.

 

BUSIA, Kenya

KATIBU msimamizi katika Wizara ya Ardhi Gideon Mung'aro amedokeza kuwa idara hiyo ya serikali inafanya kila juhudi kukamilisha usajili wa ardhi na utoaji wa hatimiliki kwa wakazi wa eneobunge la Budalang'i.

Hatua hii itatoa nafasi ya kuwafidia wakazi ambao walisalimisha vipande vyao vya ardhi kwa serikali kwa minajili ya utekelezwaji wa mradi wa unyunyizaji maji mashamba wa Lower Nzoia unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kima cha Sh10 bilioni.

“Tayari hatimiliki 8,000 ziko tayari kutolewa kwa wakazi ili kuharakisha mradi huu ambao umechelewa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Maeneo ambayo yangali na taashwishi ni Osieko, Buyofu na Bulwani ambazo stakabadhi zake zitakuwa tayari kabla ya awamu ya pili kuanzia mwezi Mei,” amesema mbunge huyo wa zamani wa Kilifi Kaskazini.

Bw Mung’aro ameyasema haya Jumatatu mjini Busia alipozitembelea afisi za Wizara ya ardhi ili kujifahamisha na wafanyikazi wa idara hiyo huku akifichua kuwa asilimia 70 ya shule za umma katika kaunti ya Busia zimepokea vyeti hivyo muhimu kupitia mradi wa 'Shule yangu'.

“Tunaendeleza shughuli hii ya kusajili ardhi ya umma hasa shule na afisi za umma ili kuzuia unyakuzi," akasema.

Mung'aro alikuwa ameandamana na Kamishna wa kaunti ya Busia Jacob Narengo na mkurugenzi wa idara ya ardhi kaunti ya Busia Tom Chepkwesi.