Wakosoa huduma 22068 ya dharura ya Nyumba 10

Joseph Kaguthi

Mwenyekiti wa Mpango wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi ahutubia wanahabari akiwa na Meja Mstaafu Rama Mwango'ombe Novemba 30, 2016. Picha/LABAN WALLOGA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, January 7   2017 at  20:24

Kwa Mukhtasari

Mwenyekiti wa mpango wa kiusalama wa Nyumba Kumi katika Kaunti ya Kirinyaga Bw Joseph Mureithi amedai kuwa afisi kuu ya kuuratibu chini ya Mkurugenzi Joseph Kaguthi imeingiwa na tamaa ya kibiashara.

 

MWENYEKITI wa mpango wa kiusalama wa Nyumba Kumi katika Kaunti ya Kirinyaga Bw Joseph Mureithi amedai kuwa afisi kuu ya kuuratibu chini ya Mkurugenzi Joseph Kaguthi imeingiwa na tamaa ya kibiashara.

Ameteta kuwa afisi hiyo huwa na mazoea ya kukataa kufuata utaratibu wa mikakati iliyowekwa ya kushirikisha mpango huo na badala yake kusisitiza biashara ya kutumiwa arafa kwa nambari spesheli ya 22068.

Akizindua nambari hiyo ya dharura mwishoni mwa mwaka 2015, Bw Kaguthi alisema kuwa “ni ya kutusaidia kupiga jeki mikakati ya kiusalama ambapo wasiojua kwa kupiga simu wakikumbana na ujambazi wanaweza wakatutumia sisi ili tuusambaze kwa vitengo mwafaka.”

Arafa hiyo humgharimu anayeituma na kwa kawaida makampuni ya huduma za simu za mkononi huwa wanahesabia wamiliki wa nambari hizo marupurupu ya usajili na utumiaji.

“Afisi hiyo imezindua nambari ya arafa ambayo kwa sasa inauzwa kupitia kwa matangazo ya kibiashara mashinani. Ni ujumbe mfupi ambao unafaa kutumwa kwa nambari hiyo kutoka kwa wananchi bali sio katika utaratibu wa kiutawala,” akasema.

Alisema kuwa kamati za mashinani za mpango huo zinafaa kushirikiana na machifu, wakuu wa tarafa, Naibu wa Kamishna na makamishna ili mikakati iandaliwe katika kikao rasmi cha kamati ya kiusalama ya Kaunti.

"Ilivyo kwa sasa, mwananchi akishuhudia lolote lenye shaka kiusalama anaambiwa achape arafa harakaharaka hadi katika nambari hiyo. Wakati unaotumika kuandika arafa hiyo unafaa kutumika kuitisha usaidizi wa dharura karibu na raia huyo,” akasema.

Bw Mureithi akiongea Mjini Ngurubani alisema kuwa “ikiwa serikali kwa dhati inaelewa kuwa inataka kuwasaidia wakenya, basi ingetoa huduma kama hiyo bila gharama yoyote sawa na vile nambari zingine za dharura kuhusu ujambazi na majanga huwa hazitozi ada yoyote.”

Akasema: “Hii ni biashara ya arafa na hivi karibuni huenda tuone Bw Kaguthi na washirika wake wakizindua huduma nyingine ya kamari ambapo utaambiwa ubahatishe kama kwenu kuna uwezekano wa kushambuliwa na majambazi na kisha ujishindie zawadi.”