http://www.swahilihub.com/image/view/-/3167662/medRes/1307288/-/x4qtgz/-/nyanya.jpg

 

Wakulima wa nyanya waonywa kuhusu bei kusambaratika

Nyanya

Nyanya. Picha/HISANI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  09:46

Kwa Muhtasari

Bei za nyanya kwa sasa ziko juu.

 

MURANG'A, Kenya

WAKULIMA wa tunda aina ya nyanya katika ukanda wa Mlima Kenya wameonywa kuwa faida kubwa wanayojivunia kwa sasa itasambaratika katika kipindi kifupi kijacho.

Wameonywa kuwa msimu wa mvua kubwa ambao unaendelea kwa sasa utakuja na changamoto zake katika kilimo hicho hivyo basi kuadhili vibaya bei katika soko.

Pia, wameonywa kuwa msimu wa kijibaridi na mvua huandamana na kero la magonjwa ya mimea, hivyo basi kuongeza gharama za uzalishaji ambazo pia humeza pato na hatimaye faida.

Akihutubia warsha ya kilimo cha mboga na matunda katika mji wa Maragua ulio katika Kaunti ya Murang'a, afisa wa Usaidizi Kwa Wakulima Nyanjani wa kampuni ya Kemros Seeds, kampuni ambayo hutoa huduma za mbegu, dawa na mbolea kwa Wakulima katika eneo hilo alisema hiyo inafaa kuwa tahathari mwafaka kwa wakati huu.

Kwa sasa, bei ya zao hili imekuwa nzuri kwa soko kwani kilo moja ya nyanya inauzwa kwa Sh64 kwa soko.

“Hali hii nzuri imechangiwa na ukame uliokuwa na ambao ulikuwa umewafanya wakulima wengi kukosa maji ya kilimo hiki. Lakini mvua imeanza kunyesha na kwa mwezi mwingine ujao zao hili litafurika sokoni na kuchangia kuteremka kwa bei,” akasema.

Maradhi ya mimea

Aliongeza kuwa msimu wa mvua utapenyeza magonjwa mengi kwa kilimo cha matunda na mboga huku akionya kuwa bei ya kutunza mimea hiyo itaenda juu kutokana na madawa mengi yatakayohitajika.

“Hayo yote yatafanya bei katika soko kutokuwa na faida kubwa kwa Mkulima na ningewasihi kuwa mchanganye kilimo cha bidhaa zinginezo ambazo zitawasaidia kumudu hali ngumu ya maisha kutokana na bei duni,” akasema.