Waliochaguliwa Kiambu waanza kampeni za amani

Msafara wa Diwani

Msafara wa Diwani wa Jubilee Bw James Kimani Mburu almaarufu 'Kidim' wa wadi ya Mwiki, Kaunti ya Kiambu, ukihubiri amani mtaani Githurai 45 Ruiru, Kaunti ya Kiambu mnamo Jumamosi Agosti 12, 2017. Picha/ SAMMY WAWARU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Saturday, August 12   2017 at  14:47

Kwa Mukhtasari

Kufuatia tangazo la aliyetangazwa mshindi kiti cha urais nchini uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Jumanne Agosti 8, 2017, baadhi ya viongozi waliowania viti mbalimbali vya kisiasa na kupata ushindi Kaunti ya Kiambu wameanza kampeni za kuhubiri amani.

 

KUFUATIA tangazo la aliyetangazwa mshindi kiti cha urais nchini uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Jumanne Agosti 8, 2017, baadhi ya viongozi waliowania viti mbalimbali vya kisiasa na kupata ushindi Kaunti ya Kiambu wameanza kampeni za kuhubiri amani.

Diwani (MCA) mteule wa wadi ya Mwiki Kaunti ya Kiambu kwa tiketi ya Jubilee Bw James Kimani Mburu almaarufu Kidim, Jumamosi ameongoza msafara wake katika wadi anayowakilisha huku kibwagizo kikiwa 'Amani!Amani! Amani!'.

"Kama kiongozi, ninawakilisha makabila yote kwenye wadi ya Mwiki, nitahudumia walionichagua na ambao hawakunichagua, sisi sote ni Wakenya, tudumishe amani," kampeina wake mkuu ambaye ameomba kubana jina lake kwa sababu za kiusalama ameeleza Swahilihub akifikisha ujumbe wa MCA huyo aliyekuwa kwenye harakati za kupongeza wapiga kura kwa njia ya kipekee.

Aidha amepongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuchaguliwa tena kwa awamu ya pili na ya mwisho kuongoza taifa hili kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

"Hongera kinara wetu Mheshimiwa Kenyatta, nitashirikiana na serikali yako na ile ya kaunti kuboresha maisha ya wakazi wa wadi yangu," kampeina wa MCA Kimani amepasha ujumbe huo.

Msongamano wa magari umeshuhudiwa kwa dakika kadhaa kwenye barabara ya kutoka mtaani Githurai 45 kuelekea Mwihoko, kufuatia msafara huo uliokuwa ukihubiri amani.

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Bw Wafula Chebukati, Ijumaa usiku alitangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi baada ya kuzoa kura 8,203,290 ikiwakilisha asilimia 54.24 na kinara wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga akipata kura 6,762,224 ikiwa ni asilimia 44.92 kwa jumla ya kura 15,073,662 zilizopigwa na kuwakilisha asilimia 78.91 ya wapiga kura 19,687,563 waliosajiliwa na tume ya IEBC.

Hata hivyo, kinara wa Nasa Raila na vinara wenza wamepinga matokeo hayo wakidai kuwa si halali na kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na wizi wa kura.

Aliyekuwa mbunge wa Kabete Ferdinand Waititu ndiye gavana mteule wa Kaunti ya Kiambu kwa tiketi ya Jubilee baada ya kumbwaga gavana anayeondoka William Kabogo aliyewania kuhifadi kiti chake kama mgombea wa kujitegemea.