Jubilee yateua wabunge wanne kusimamia utendakazi wa bunge la 12

Na CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, September 13  2017 at  11:44

Kwa Mukhtasari

Shughuli za utendakazi wa bunge la 12 zimeng'oa nanga Jumatano asubuhi licha ya mvutano wa kisiasa uliopo baada ya ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee kufutiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi nchini kuagiza uchaguzi mpya ufanyike.

 

SHUGHULI za utendakazi wa bunge la 12 zimeng'oa nanga Jumatano asubuhi licha ya mvutano wa kisiasa uliopo baada ya ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee kufutiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi nchini kuagiza uchaguzi mpya ufanyike.

Jubilee Party (JP) imeteua kamati ya wabunge wanne watakaosimamia ratiba na utendakazi wa bunge la kitaifa.

Walioteuliwa ni mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya, Mwakilishi wa Wanawake Meru Bi Kawira Mwangaza, Mbunge wa Kitutu Masaba Shadrack Mose na Mwakilishi wa Wanawake Turkana Bi Joyce Emanikor.

Muungano wa National Super Alliance (Nasa) baadaye leo unatarajiwa kuwasilisha wabunge wake watakaoteuliwa.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi akiongoza kikao hicho cha awamu ya kwanza alisema sharti kazi ya bunge iendelee.

"Bunge halitaongoja walioamua kuendelea kulala. Ndege anayerauka mapema ndiye humla mchwa," amesema Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi Jumatano wakati akiendesha mjadala huo.

Akaongeza: "Biashara ya bunge sharti iendelee."

Kujitetea

Licha ya wabunge wa upinzani, NASA, kudinda kuhudhuria kikao cha ufunguzi rasmi wa Bunge la 12, wenzao wawili walikaidi msimamo huo.

Mbunge wa Webuye Mashariki Alfred Sambu na mwenzake wa Hamisi Charles Gimose walihudhuria shughuli iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Kwenye mahojiano ya wanahabari baada ya ufunguzi huo Bw Sambu ambaye alichaguliwa bungeni kwa tiketi ya Chama cha Amani National Congress (ANC) alisema hangekosa shughuli hiyo kwa sababu ni shughuli ya kitaifa ambayo haifai kuingizwa siasa.

"Sherehe ya ufunguzi wa bungeni kwa sababu hii ni shughuli muhimu ambayo sisi kama wawakilishi wa raia tunafaa kuchukulia kwa umuhimu mkubwa. Nimehudhuria shughuli hii kwa sababu ni ya kitaifa na mimi kama mwakilishi wa watu wa Webuye Magharibi ilibidi nihudhurie," akasema Bw Sambu ambaye zamani alikuwa Mwenyekiti wa Shirikisho wa Soka Nchini (KFF).

Naye Bw Gimose ambaye pia ni Mbunge wa chama cha ANC kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi, alisema amekuwa mashinani na hakuwa na habari kwamba wabunge wenzake wa upinzani waliafikiana kususia bungeni.

"Nimekuwa nyumbani nikiwapongeza wapigakura wangu kwa kunichagua. Nilipata habari kuhusu kufunguliwa kwa bunge lakini sikupata habari kwamba wenzangu waliamua kususia kikao cha leo kwa sababu moja ama nyingi," akasema Gimose ambaye anahudumu kwa kipindi cha pili.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

mwanzo| Habari| Jifunze Kiswahili| Blogu Na Ukumbi| MAKTABANI JISOMEE| picha| video| Makala|