KINAYA: Aibu ya wanasiasa waliojitanua vifua kukodolea macho kichapo

Uhuru Raila

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wakiwa Ikulu, Nairobi. Picha/PSCU 

Na DOUGLAS MUTUA

Imepakiwa - Sunday, August 6   2017 at  14:17

Kwa Mukhtasari

HAYAWI hayawi huwa! Vidomodomo ambavyo umeshuhudia katika muda wa takribani miaka miwili vimekukoma sasa.

 

La, bora zaidi ni kusema vimekomeshwa. Unaweza pia kusema vimepumzika kwa muda kisha kazi ya kupiga kelele iendelee.

Siamini kwamba wanasiasa wametulia kiasi hiki kutokana na sheria inayowataka wahitimishe kampeni zao saa 48 kabla ya siku ya uchaguzi. La hasha!

Wamefyata ndimi kwa maana wameingia baridi kupindukia, kila mmoja akiwaza na kuwazua itakuwaje iwapo atabwagwa katika uchaguzi utakaofanyika Jumanne ya kesho kutwa.

Ujeuri ulioshuhudia wakati wa kampeni - kila mwaniaji akitanua kifua kukwambia atakavyoshinda huku akimtishia mpinzani wake umeondoka nyoyoni za wengi na pahali pake pakaingia woga, wasiwasi - mkururo wa mawazo…

Iwe ni ama 'Baba’ na 'Watermelon’ wake, 'Ithe wa Jaba’ na Arap Mashamba au wawaniaji wengine wa nyadhifa ndogondogo, wasiwasi umemkumba kila mtu akijiuliza maswali chungu nzima.

Mathalan, japo kajiamini kabisa mbele ya watu kwamba atashinda uchaguzi huu asubuhi – kana kwamba siku hizi kura huhesabiwa asubuhi kabla ya vituo kufungwa – 'Ithe wa Jaba’ anajiuliza akishindwa itakuwaje!

Kwake ushindi ni rahisi kuliko ushinde kwa maana itakuwa kuendelea tu na kazi aliyozoea. Bila shaka atajitapa mbele ya kila mtu, akukumbushe: Nilikwambia sishindiki nikiwa afisini; niliwashinda nikiwa msituni enzi hizo, tena nikikabiliwa na kesi mbele ya Wazungu, seuze mara hii nikiwa mwenyeji wa ikulu.

Kibarua kigumu kwake na Arap Mashamba kitakuwa kukubali matokeo iwapo watashindwa.

Ikiwa wewe ni mtu wa Nasa, nina hakika unasema hawana chaguo ila kung’atuka wakishindwa, eti uamuzi si wao kudumu mamlakani au kuondoka, mradi wananchi wameamua.

Bila shaka sheria inasema hivyo, mshinde afunganye na kuelekea kwao alikotoka. Lakini si rahisi inavyotamkika. Usicheze na kisa cha mla-nyama kugeuka mmeza-mate, akarithiwa na aliyekuwa mmeza-mate.

Nakumbuka vyema alivyolia kilio kisichozuilika Samoei Kipchirchir baada ya muungano wa chama cha The National Unity (TNA) na United Republican Party (URP) kutangazwa washindi wa Uchaguzi Mkuu wa 2013.

Ikiwa muungano wake wa Jubilee utabwagwa mara hii, usitarajie ajitokeze hadharani kulialia kama kitoto cha chekechea kilichopokonywa peremende.

Matokeo yakiwa ushinde, wanaojiamini kama wanaume kamili hulilia kwa wake zao! Baadaye hujitokea huku kakaza uso utadhani hawajui hata tone moja na machozi. Kilio cha hadharani huwa cha kusherehekea ushindi.

Ikiwa 'Baba’ atabwagwa tena wakati huu – kwa mara ya mia ngapi sijui… - bila shaka atatumia tajiriba yake ya miaka mingi ama kulia kwa sauti kuu kama mvulana mwoga aliyefanya marejeo kwa ngariba.

Huenda hata asiweze kujizuia, aangue kilio kikuu hadharani mbele ya kamera za runinga, arudie kibwagizo chake cha tangu jadi: Wameiba kura zangu.

Hata 'Baba’ asipolia hadharani, huenda Watermelon akafanya hivyo akikumbuka safari ndefu atakayofunga kuelekea kijiji kikavu cha Tseikuru alikotoka akija kujaribisha bahati mjini ila akashindwa kuwika.

Natarajia asaidiwe kulia kwa sauti kuu na Elizabeth Ongoro na Millie Odhiambo mtukana watu, huyu wa mwisho aseme 'wajinga’ wameiba tena.

Ila hali itakuwa shwari kwa 'Baba’ akishinda: Kicheko cha bashasha, ahadi ya kupatanisha nchi, sikwambii kelele za wananasa barabarani!

 

mutua_muema@yahoo.com