Wanne waliouawa na Al-Shabaab wazikwa Mpeketoni

Na KALUME KAZUNGU

Imepakiwa - Wednesday, September 13  2017 at  15:50

Kwa Mukhtasari

Huzuni ilitanda Jumanne jioni katika vijiji vya Bobo na Ndeu tarafa ya Hindi na Uziwa, tarafa ya Mpeketoni kwenye mazishi ya watu wanne waliouawa na magaidi wa Al-Shabaab juma moja lililopita.

 

HUZUNI ilitanda Jumanne jioni katika vijiji vya Bobo na Ndeu tarafa ya Hindi na Uziwa, tarafa ya Mpeketoni kwenye mazishi ya watu wanne waliouawa na magaidi wa Al-Shabaab juma moja lililopita.

Wanne hao waliuawa kwa kuchinjwa pale washukiwa zaidi ya 30 wa Al-Shabaab waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari kuvamia vijiji vyao mnamo usiku wa Septemba 6.

Waliozikwa ni pamoja na mwalimu wa shule ya msingi ya Bobo, Bw Joseph Kinuthia Kimani, Bw Gerald Wagunyi Wanjahi, Bw Samuel Ngushu Ndung’u na Bw Hilary Kiara.

Wanne hao walizikwa katika mazishi yalioyoshuhudia ulinzi mkali wa maafisa wa usalama wakiwemo polisi na wanajeshi wa KDF.

Viongozi mbalimbali wa kaunti ya Lamu akiwemo Gavana Fahim Twaha na wakuu wa idara ya usalama eneo hilo walihudhuria mazishi hayo.

Akihutubia waombolezaji waliojitokeza katika kijiji cha Bobo, Bw Twaha alitoa wito kwa serikali ya kitaifa kukabiliana vilivyo na magaidi wa Al-Shabaab ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi kila kukicha eneo hilo.

Alisema serikali ya kaunti ya Lamu itajitolea kikamilifu na kushirikiana na serikali ya kitaifa katika kukabiliana na kumaliza uhalifu eneo hilo.
Alisema hivi karibuni atajadiliana na Rais Uhuru Kenyatta ili kuona kwamba idadi ya askari wa akiba inaongezwa kote Lamu ili kusaidia katika kukabiliana na kero la Al-Shabaab.

“Kwa mara nyingine tena tunahuzunika kwa kupoteza wenzetu wanne kupitia uvamizi wa Al-Shabaab. Wakati umewadia kwa serikali kuu kuhakikishia raia usalama bila kusahau mali eneo hili. Kama kaunti, tuko tayari kushirikiana vilivyo na serikali kuu ili kurejesha amani na utulivu eneo hili. Tumechoka kupoteza watu wetu. Ombi langu kwa serikali pia ni kuhakikisha KPR wanaongezwa Lamu ili kukabiliana na magaidi wanapovamia vijiji vyetu,” akasema Bw Twaha.

Waombolezaji wengi waliohudhuria mazishi hayo pia waliililia serikali kudhibiti zaidi usalama kote Lamu ili kuepuka maafa zaidi yanayotekelezwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Wakazi waliiomba serikali kubuni vituo vingi zaidi vya polisi kwenye maeneo yote ambayo yamekuwa yakilengwa na Al-Shabaab, ikiwemo Hindi, Witu, Basuba, Kiunga, Ishakani, Maleli, Pandanguo, Jima na Poromoko.

“Serikali iimarishe usalama eneo hili. Doria za walinda usalama ziongezwe. Vituo vya polisi na jeshi pia viongezwe. Sisi pia tumejitolea. Serikali itupe mafunzo na bunduki ili kujilinda vijijini mwetu,” akasema Bw William Mwangi.

Wakuu wa usalama waliohudhuria mazishi hayo waliwahimiza wakazi kwa kudumisha ushirikiano na polisi na kuwa tayari kutoa ripoti zitakazosaidia kukabiliana na wahalifu.

Waliwataka wakazi kuondoa hofu na badala yake waishi kwa amani, wakisisitiza kuwa walinda usalama wa kutosha wamesambazwa kwenye maeneo yao ili kudhibiti usalama wa raia na mali.