Wafanyabiashara Thika wapinga kufurushwa kutoka eneo lao la biashara

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Tuesday, February 13  2018 at  12:04

Kwa Muhtasari

Wafanyabiashara 500 wanaofanyia shughuli zao kando ya barabara kuu ya Thika-Garissa eneo la Gatito, waliandamano mnamo Jumatatu wakipinga kufurushwa katika maeneo hayo.

 

WAFANYABIASHARA 500 wanaofanyia shughuli zao kando ya barabara kuu ya Thika-Garissa eneo la Gatito, waliandamano mnamo Jumatatu wakipinga kufurushwa katika maeneo hayo.

Walimlaumu diwani mmoja wa Kaunti ya Kiambu ambaye wamesema anatumia mamlaka yake visivyo ili kuwanyanyasa.

Walizidi kuteta ya kwamba mwanasiasa huyo ameshirikiana na Halmashauri ya usalama wa usafiri KeNHA, ili kuwafurusha.

Hapo awali maafisa fulani walitumwa katika sehemu hiyo ambapo waliweza kubomoa vibanda vilivyotundikwa katika sehemu hiyo. Kwa sasa wengi wamebaki katika mahangaiko makubwa.

Akieleza wanahabari kadhia, Bi Roseline Karwitha, ambaye anaendesha biashara yake hapo alisema watu fulani wamekuwa wakizuru mahali hapo tangu mwezi Oktoba 2017.

"Sisi wafanyabiashara tulishuku malengo yao hapo. Mara nyingi wakija huzunguka eneo hilo bila kuzungumza na yeyote, jambo linalofanya tuwe na hofu," alisema Bi Karwitha.

Kulingana na wafanyabiashara ni kwamba wanashuku maafisa wakuu katika Kaunti ya Kiambu wana siri fiche kuhusu kufurushwa kwao kutoka mahali hapo.

Walisema hivi majuzi watu wasiojulikana walibomoa vibanda kadha na kuharibu mali yenye thamani ya takribani Sh200,000.

"Sisi tunaiomba Kaunti ya Kiambu iwe wazi na sisi wafanyabiashara na iketi chini nasi. Wanafaa kutueleza ni mipango ipi walio nayo na wanataka tuelekee wapi," alisema Bi Karwitha.

Walisema wao ni watu walio na familia zao na hawangetaka kuhangaishwa hivyo kila mara.

Pia walizidi kueleza kuwa wana leseni halali za kuendesha biashara yao hapo.

Inadaiwa kuwa kuna watu fulani ambao pengine wanataka kukodisha sehemu hiyo ili wazidi kufanya biashara zao hapo.

Eneo hilo ni kando ya barabara unapoingia mji wa Thika.

Sehemu hiyo kulingana na wafanyabiashara hao ni kama mita 300 kwa urefu na lina wateja wengi wanaofika hapo kununua bidhaa tofauti.

Baadhi ya vitu muhimu vinavyouzwa mahali hapo ni vyandarua, viti, samadari, miche ya maua ya kupanda, na vinyago vya mawe.

Juhudi ya Swahili Hub kutaka kupata taarifa kamili kutoka afisi kuu ya Kaunti ya Kiambu ziligonga mwamba kwa sababu hakuna aliyeshika simu kupokea.