Watendaji wa Serikali Zanzibar mtegoni

Na MUHAMMED KHAMIS, Mwananchi

Imepakiwa - Tuesday, January 29  2019 at  12:41

Kwa Muhtasari

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt Khalid Salum Mohamed amewaagiza watendaji wa Serikali kuacha kuzusha vyanzo vipya vya mapato.

 

UNGUJA

WAZIRI wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt Khalid Salum Mohamed ameonyesha kukerwa na watendaji wa Serikali kuongeza vyanzo vya mapato hivyo kumuongezea mwananchi mzigo, huku akiwataka kuacha tabia hiyo mara moja.

Aliyasema hayo kwenye kikao cha kuibua mambo ya kuzingatia katika utayarishaji bajeti kwa mwaka 2019/20 kilichowashirikisha watendaji wakuu wa Serikali, serikali za mitaa na taasisi zinazohusiana na ukuaji wa uchumi.

Dkt Khalid alisema lengo la kikao hicho ni utekelezaji wa sheria namba 12 ya mwaka 2016 ambayo inataka kuanzishwa kwa jukwaa la bajeti na uchumi.

Alisema miongoni mwa maeneo yanayohitajika kupitiwa upya ni hali ya uchumi; mfumo wa mapato; vyanzo vya mapato vinavyofanya kazi; matumizi ya fedha na changamoto zilizopo.

Pia, alisema kutakuwa na utaratibu wa kuangalia sekta tatu zilizogatuliwa ikiwamo elimu, afya na kilimo ili kuhakikisha kunakuwa na urahisi wa upelekaji huduma za jamii na kufikia malengo ya Serikali.

Eneo jingine ni uhaulishaji fedha kwa taasisi zilizogatuiliwa, ambao unapaswa kufanywa kwa kuzingatia vigezo ikiwamo idadi ya watu.

Sambamba na hilo, Dkt Khalid alisema eneo jingine litakaloangaliwa kwa umakini ni hali ya umaskini katika utafiti wa kaya uliofanywa mwaka 2014/15.

Kuhusu rasilimali watu wenye ujuzi, alisema kamati maalumu imeundwa kuangalia eneo hilo na kupatiwa ufumbuzi sambamba na kamati ya kuangalia sheria na mahitaji ya fedha.

Naye katibu mkuu wa wizara hiyo, Khamis Mussa Omar alisema ugatuzi ni miongoni mwa eneo muhimu la kufanyiwa tathmini ya haraka na kuangalia changamoto zilizopo.

Khamis alisema ugatuzi ni njia mojawapo ya hatua za kuharakisha upelekaji huduma kwa jamii hivyo linahitaji kutekelezwa kwa weledi.

 

Maoni na mapendekezo

Awali, kamishna wa bajeti, Mwita Mgeni Mwita alisema kikao hicho kimepokea maoni na mapendekezo yatakayoingizwa katika bajeti ambayo itapelekwa Baraza la Mapinduzi na baadaye Baraza la Wawakilishi.

Akichangia katika kikao hicho, Saleh Haji kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alipendekeza kuandaliwa mfumo maalumu wenye kudhibiti mapato katika bandari bubu.