Wachunguzi wa UN warejea Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akihutubia wanahabari awali. Picha/AFP 

Imepakiwa - Wednesday, September 25  2013 at  13:12

Kwa Muhtasari

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa (UN) walirejea Syria Jumatano, kuendeleza uchunguzi kuhusu madai ya utumizi wa silaha za kemikali kwenye mashambulizi.

 

DAMASCUS, Syria

WAPELELEZI wa Umoja wa Mataifa (UN) walirejea Syria Jumatano, kuendeleza uchunguzi kuhusu madai ya utumizi wa silaha za kemikali kwenye mashambulizi, huku Urusi na mataifa ya magharibi zikipingana kuhusu jinsi ya kumpokonya Bashar al-Assad, silaha za kemikali zilizopigwa marufuku kimataifa.

Kikosi hicho kilichoongozwa na mtaalamu mkuu Ake Sellstrom, kiliwasili katika uwanja wa ndege wa Beirut kabla kusafiri kwa msafara wa magari na kuvuka hadi Syria, kulingana na mpigapicha wa shirika la AFP aliyekita kambi katika eneo la mpaka wa Masnaa.

Rais wa Amerika Barack Obama, Jumanne aliagiza Baraza la Usalama lichukue hatua kali dhidi ya Syria huku mapigano yanayoendelea katika nchi hiyo yakijadiliwa pakubwa kwenye kongamano la Umoja wa Mataifa.

Kikosi cha Sellstrom kinatarajiwa kukagua madai ya matumizi ya silaha za kemikali takriban mara 14, kwenye makabiliano ya miezi 30 yanayosemekana yalipelekea kufariki kwa zaidi ya watu 110,000.