Watoto wa kurandaranda mitaani Uganda hudhulumiwa kimapenzi – Ripoti

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Friday, July 18  2014 at  14:34

Kwa Muhtasari

Shirika la Haki za Binadamu 'Human Rights Watch’ limesema  watoto wasio makao wanaoishi mijini nchini Uganda huwa wanakabiliwa na ghasia, ikiwa ni pamoja na dhuluma za kimapenzi kutoka kwa polisi na raia.

 

KAMPALA, Uganda

SHIRIKA la Haki za Binadamu 'Human Rights Watch’ limesema  watoto wasio makao wanaoishi mijini nchini Uganda huwa wanakabiliwa na ghasia, ikiwa ni pamoja na dhuluma za kimapenzi kutoka kwa polisi na raia.

Katika ripoti iliyotolewa Alhamisi, shirika hilo lilisema kuwa mamlaka za taifa hilo zimeshindwa kuwalinda watoto hao kutoka kwa polisi huku wakaazi wa mijini wakiwachapa na kuwanyang’anya fedha.

Shirika hilo lilisema kuwa watoto hao huwa wanazuiliwa katika seli moja na watu wazima baada ya operesheni ambazo kikawaida huwa zikiwalenga.

Watoto hao wapo kwa wingi katika barabara za mji wa Kampala, ambako huwa wanaombaomba kutoka kwa waendesha magari na wengi wao ni wasichana wenye watoto wachanga.

Msemaji mmoja wa polisi, Patrick Onyango alisema  madai hayo si ya kweli, akishikilia kuwa ni watoto walio zaidi ya miaka 18 huwa wanakamatwa.

“Habari hizo ni za uongo. Kamwe hatuwezi kuwakamata watoto walio na umri wa chini kama inavyodaiwa,” akasema Bw Onyango.