http://www.swahilihub.com/image/view/-/2450832/medRes/828886/-/xyoympz/-/158516-01-02.jpg

 

Kampuni za Kenya kusaidia kuchangisha pesa za Ebola

Ivory Coast

Shabiki wa timu ya taifa ya soka ya Ivory Coast akiwa na bango lisemalo "Stop Ebola" (Zuia Ebola), wakati wa mechi kati ya Ivory Coast na Sierra Leone uwanja wa Felix Houphouet-Boigny, Abidjan Septemba 6, 2014. Picha/AFP 

Na WYCLIFFE MUIA

Imepakiwa - Wednesday, December 3  2014 at  16:41

Kwa Muhtasari

Kampuni za mawasiliano za Safaricom, Airtel na Orange zimezindua mpango wa kufadhili juhudi za kupambana na Ebola katika mataifa ya Afrika Magharibi.

 

KAMPUNI za mawasiliano za Safaricom, Airtel na Orange Jumatano zilizindua mpango wa kufadhili juhudi za kupambana na Ebola katika mataifa ya Afrika Magharibi.

Mpango huo ambao unaongozwa na Muungano wa Afrika (AU) utatumia huduma za sms katika mitandao yote ya mawasiliano nchini.

“Kila ujumbe utagharimu Sh20 ambazo zitakusanywa na AU na kugawiwa mataifa ya Afrika Magharibi ambayo yameathiriwa na maradhi hatari ya Ebola,” alisema Bw Joseph Ogutu, Afisa wa Operesheni katika kampuni ya Safaricom.

Bw Ogutu alisema kuwa kando na kushiriki katika mpango huo, Safaricom itasaidia kusambaza jumbe za tahadhari ya Ebola miongoni mwa wateja wake.

“Tumefaulu katika mipango sawia kama vile Kenyans for Kenya na wakati umewadia kupanua ukarimu wetu kwa ndugu zetu wa Afrika Magharibi wanaohangaishwa na Ebola,” alisema Bw Ogutu.

Vincent Lobry, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Orange alisema kuwa wanaoshiriki watatuma ujumbe 'Stop Ebola’ kwa nambari 7979.

“Unaweza kutuma sms ukiwa katika mtandao wowote ule na tunahimiza Wakenya kutuma mara nyingi iwezekanavyo,” alisema Bw Lobry.

Kulinda wateja

Naye Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Airtel, Shivan Bhargava alisema kuwa mpango huo utasaidia AU kutuma maafisa zaidi Afrika Magharibi ili kupambana na janga hilo.

“Sisi kama kampuni za mawasiliano tuna jukumu la kuwalinda wateja wetu ndani na nje ya nchi. Ufanisi wa mpango huu utategemea sana kushiriki kwa wateja wetu ambao wamedhihirisha kuwa na ukarimu awali,” alisema Bw Bhargava.

Kupitia Afisa mkuu wa kuzuia na kukinga maradhi nchini Jackson Kioko, serikali ilisifu hatua ya kampuni hizo na kuahidi kutoa usaidizi zaidi wa kitaaluma katika mataifa yaliyoathiriwa na Ebola.