S. Korea kuzungumza na N. Korea kuondoa taharuki ya kinuklia

Na AFP

Imepakiwa - Monday, July 17  2017 at  15:40

Kwa Mukhtasari

KOREA Kusini Jumatatu ilisema kwamba iko tayari kuandaa mazungumzo ya kijeshi na Korea Kaskazini, ili kuondoa taharuki iliyopo baada ya taifa hilo (Korea Kaskazini) kufanya majaribio ya silaha za kinuklia.

 

Tangazo hilo ndilo la kwanza tangu Moon Jae-In kuchaguliwa kama rais mpya wa taifa hilo.

Shirika la Msalaba Mwekundu (RC) nchini humo pia limependekeza mkutano tofauti kujadili kuhusu utaratibu za kuziunganisha familia ambazo zilitenganishwa na vita kati ya mataifa hayo mawili kati ya 1950 na 1953.

Wizara ya Ulinzi ya Kusini ilipendekeza mkutano huo kufanyika mnamo Ijumaa katika kijiji cha mpakani cha Panmunjom, huku RC ikiomba kuendesha mazungumzo hayo mnamo Agosti 1 katika eneo lilo hilo.

Ikiwa mkutano uliopendekezwa na serikali utafaulu, itakuwa mara ya kwanza kwa nchi hizo mbili kuandaa mazungumzo tangu Desemba 2015. Mtangulizi wa Rais Moon, Park Geun-Hye, alikataa kushiriki katika mazungumzo yoyote na Kaskazini, akilitaka kusitisha kabisa mpango wake wa utengenezaji na majaribio ya silaha hizo hatari.

“Tunatangaza pendekezo la kuandaliwa kwa mkutano…tukilenga kuondoa masuala yote ambayo yamekuwa yakizua mgawanyiko kati yetu. Tunataka kupunguza taharuki ya kijeshi inayoendelea kuongezeka katika maeneo ya mpakanik,” ikasema wizara hiyo kwenye taarifa.

Shirika la Msalaba Mwekundu lilisema kwamba linatarajia “majibu mazuri” kutoka kwa Kaskazini, ili kuziwezesha familia hizo kuungana tena kufikia mapema mwezi Oktoba. Ikiwa mazungumzo hayo yatafaulu, yatakuwa ya kwanza katika muda wa miaka miwili.

Mamilioni ya familia yalitenganishwa na vita hivyo vilivyopelekea kutengana kwa nchi hizo mbili.

Wengi walifariki bila ya kupata nafasi ya kuwaona au kutangamana na familia zao kutokana na ulinzi mkali uliowekwa katika mpaka huo. Raia hawakuruhusiwa kuvuka mpakani.

Na kadri muda ulivyosonga idadi ya manusura imeendelea kupungua, huku ikikisiwa kwamba kufikia sasa wamebaki 60,000 wengi wakiwa Kusini.

“Korea Kaskazini inapaswa kulikubali ombi letu, ikiwa inataka hali ya amani kurejea katika ukanda huu,” akasema Waziri wa Masuala ya Muungano Cho Myoung-Gyon, kwenye kikao na wanahabari.

Cho alisisitiza kwamba lengo lao si “kuisambaratisha Kaskazini” ila ni kurejesha mawasiliano na ushirikiano kati yao.

Moon, aliyechukua uongozi mnamo Mei, amekuwa akisititiza uwepo wa mashauriano ili kurejesha mahusiano mazuri kati yake.

Licha ya juhudi hizo, Kaskazini inaonekana kutotilia maanani rai hizo, ikiendelea na majaribio ya silaha zake. Mnamo Julai 4, ilifanya jaribio la kombora maalum aina ya ICBM, hali ambayo ilikosolewa vikali nan chi mbalimbali duniani pamoja na Rais Donald Trump wa Amerika.

Katika kujaribu kutuliza hali, Amerika imeiomba Uchina kuirai Kaskazini kusitisha utengenezaji wa zana hizo.