Swaziland yatumia miaka 50 kuitwa eSwatini

 

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  07:58

Kwa Mukhtasari

Wakati sherehe ya miaka 50 ya Mfalme Mswati III ikikaribia Aprili 19, 2018 ishara zote ziliashiria kwamba kuna jambo kubwa lililokuwa likienda kutokea.

 

Mbabane, Swaziland. Wakati sherehe ya miaka 50 ya Mfalme Mswati III ikikaribia Aprili 19, 2018 ishara zote ziliashiria kwamba kuna jambo kubwa lililokuwa likienda kutokea.

Kulikuwa na kila dalili kwamba mfumo wa maisha ya Waswazi ulikuwa unabadilika, ingawa sio kisiasa, lakini katika utambulisho wao, kama Waswazi. Ilikuwa ni dhahiri kwamba jina la Taifa hilo dogo lililopo Kusini mwa Afrika linabadilika na kupata jipya.

Pia, zilikuwapo hisia mbalimbali kuhusu Mswati wakati akielekea kuadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwake iliyofanyika Aprili 19, kuwa angeoa wake wawili au watatu kwa mpigo, tofauti na taratibu za kimila alizorithi kutoka kwa baba yake, Mfalme Sobhuza II aliyekuwa akioa mke mmoja. Hata hivyo haikuwa hivyo.

Badala yake, Mswati III aliyezaliwa mwaka 1968, miezi mitano kabla ya Taifa hilo lililopo Kusini mwa Afrika halijapata uhuru Septemba 6, alitumia siku hiyo kubadili jina la nchi na kuiita eSwatini badala ya Swaziland.

Licha ya kufanya hivyo, lakini mfalme huyo ni kama alitaka sherehe za Septemba 6 ziende sambamba na siku yake ya kuzaliwa iliyokuwa mahsusi kwake kwa ajili ya kubadili jina la nchi. eSwatini linamaanisha kuwa nchi ya Waswati.

Siku hiyo iliambatana na shamrashamra za aina mbalimbali, ofisi za umma na binafsi kufungwa kama siku ya mapumziko na pia majeshi na vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama kufanya maandamano mitaani.

Hata hivyo, yote hayo aliyafanya kwa tahadhari na hakutaka hata mtu mmoja aone kuwa ufalme wake haupaswi kutenganishwa na Swaziland, kwa maana ya kuwa kila asemacho ni amri na itekelezwe hata kama inapingana na demokrasia ya majadiliano kupitia Bunge na Seneti.

Mbali na hilo, Mswati alilenga kupandikiza vichwani mwa watu kwamba ‘besidei’ yake ya kutimiza miaka 50 ina uhusiano mkubwa na jubilee ya miaka 50 ya uhuru wa Taifa hilo, na kwa pamoja Waswazi wanapaswa kuzisherehekea kwa siku moja. Baada ya kuhisi upinzani wa chinichini juu ya dhamira yake hiyo, mfalme huyo alitoa tangazo kwamba hakuwa na mpango wa kuongeza mke, isipokuwa alitaka kubadili jina la nchi iliyokuwa ikifahamika kama Jamhuri ya Ufalme wa Swaziland sasa kuitwa Ufalme wa eSwatini.

Majina mengine yaliyotikisa

Mabadiliko ya majina katika nchi mbalimbali barani Afrika yamekuwa na changamoto, lakini wananchi wamekuwa wakiyapokea na kuyazingatia. Hata hivyo kuna mengine ambayo yamekuwa yakipokewa kwa hisia tofauti.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo

Nchi hiyo inayopakana na Tanzania upande wa Magharibi, ilibadili jina lake miezi michache baada ya utawala wa Mobutu Seseseko kupinduliwa na Laurent Desire Kabila mwaka 1997.

Hata hivyo katika kutoka jina la awali la Zaire, Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo maarufu kama DRC yenye wakazi milioni 84.7 (kwa mujibu wa Sensa ya Watu ya mwaka 2016), haikukumbana na upinzani wowote wa wananchi, licha ya kwamba wapo waliopinga wakiamini matumizi ya lile la zamani (Zaire) yalikuwa yamezoweleka.

Itakumbukwa kwamba kabla ya kubadilishwa jina hilo na Kabila (ambaye ni baba mzazi wa rais wa sasa), na pia kuitwa Zaire (kati ya 1971 hadi 1997) na Mobutu, huko nyuma DRC ilifahamika kama Belgian Congo miaka 1870 ilipokuwa chini ya Mfalme Leopold II wa Ubelgiji.

Zimbabwe

Kabla ya uhuru, Aprili 18, 1980, Zimbabwe iliwahi kuitwa Southern Rhodesia (1898), Rhodesia (1965) na Zimbabwe Rhodesia (1979). Asili ya jina Zimbabwe ina uhusiano wa karibu na mpigania uhuru wa zamani wa nchi hiyo, Michael Mawema.

Kwa mujibu wa Mawema, jina ‘Zimbabwe’ lilitokana na mapendekezo yaliyotolewa na wapigania uhuru katika miaka ya 1960 ambao awali walipendekeza nchi hiyo iitwe Matshobana au Monomotapa.

Hata hivyo, kwa Wazimbabwe wengi jina hilo walilifurahia kwa sababu lilitokana na wazalendo, tofauti na Rhodesia lililotokana na wakoloni wa ukoo wa Mwingereza, Cecil Rhodes.

Ghana

Ghana ambayo awali ilifahamika kama Gold Coast ilibadili jina siku ya uhuru Machi 6, 1957. Nchi hiyo ilikuwa jamhuri Julai 1, 1960 na ilikuwa ni mwaka huo ambapo umaarufu wa jina Ghana ulisambaa duniani. Kabla ya kipindi hicho, ilichukua miaka 50 kwa Ghana kufikia hatua ya kuitwa hivyo.

Nchi nyingine iliyotikisa kwa jina lake ni Botswana ilipobadili jina kutoka kuitwa Bechuana, ambapo ilifanya hivyo siku ya uhuru wake, Septemba 30, 1966 ilipojiondoa mikononi mwa Waingereza.

Zingine ni Malawi ambayo hadi siku ya uhuru wake Julai 6, 1966 ilikuwa ikiitwa Nyasaland, huku Zambia iliitwa Northern Rhodesia.

Wakosoaji wa Swaziland

Watu wanaomkosoa Mfalme Mswati III wanasema alichokifanya kubadili jina la nchi hiyo katika kipindi hiki hakiakisi uzalendo kwa Taifa lake, wakimtajia mwanamapinduzi wa Burkina Faso, Thoma Sankara aliyeingia madarakani mwaka 1983 na kuukata ‘utumwa’ wa kutumia jina la Kizungu la Upper Volta.

Watu hao wanadai kuwa Sankara aliwatendea haki wananchi wake kabla ya kuuawa mwaka 1984. Jina Burkina Faso linaamanisha kuwa ni ‘ardhi la watu wasiokula rushwa.’

“Mfalme Mswati III alitaka tu dunia nzima ijue kwamba ametimiza miaka 50, lakini hakumaanisha kingine zaidi ya hicho ndiyo maana hadi sasa jina hilo (eSwatini) halionekani kuchangamkiwa na watu,” anasema mkazi wa Mbambane, Motswane Konger.

Maijul Nuoye anasema kwa kuwa utawala wa eSwatini yenye watu milioni 1.3 ni wa kifalme, hakuna namna ambavyo wananchi wanaweza kubadili demokrasia ya mtu mmoja kuamua mambo yanayoathiri maisha ya wengi.

“Hili jina wala halikupita bungeni, alilisherehesha yeye mwenyewe (mfalme) na ndiyo maana kinachoendelea ni kama kumshangaa. Huyu ni kiongozi wa kiimla ambaye anapaswa kubadilika badala ya kufanya mambo kwa kukurupuka,” anasema Igjiul Kongly, mkazi wa Lombamba nchini humo.