Siri nyuma ya pazia uokoaji wa waliokwama kwenye pango

Watoto waliookolewa katika pango Kaskazini mwa Thailand wakiwa hospitali 

Imepakiwa - Friday, July 13  2018 at  08:51

Kwa Muhtasari

Kijana mmoja ndiye aliyetoa mchango mkubwa kufanikisha uokoaji

 

Bangkok, Thailand. Kijana mmoja mzaliwa wa Myanmar mwenye miaka 14 ambaye alikuwa miongoni mwa watoto 12 walionaswa pangoni Kaskani mwa Thailand amejitokeza kuwa shujaa baada ya kutajwa ndiye aliyetoa mchango mkubwa kufanikisha operesheni za uokoaji huo kuwa rahisi.

Kijana huyo Adul Sam-on ambaye utotoni mwake alipitia maisha ya taabu ikiwamo kutelekezwa alikuwa kiunganishi cha mawasiliano ya lugha kati ya wazamiaji wa mataifa ya nje na wale wa Thailand.

Anatajwa kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha zaidi ya tano. Ndiye alikuwa na uwezo wa kuwasiliana kwa lugha ya Kiingereza na wazamiaji wa Uingereza ambao ndiyo waliowagundua kwa mara ya kwanza watoto hao tangu watoweke machoni mwa watu.

Watoto hao waligundulika siku kumi baadaye wakati wazamiaji hao walipokuwa kwenye msako ndani ya pango hilo.

“Mtoto huyo ambaye yuko katika ari kubwa na afya njema ndiye aliyefanya mawasiliano ya kwanza na wanamaji wa Uingereza wakati waokoaji hao walipowagundua watoto hao wakiwa wamenasa kwa siku kumi kwenye pango.

Ufahamu wake wa lugha nyingi ikiwamo Kiingereza ndiyo uliorahisisha mawasiliano na hata kufanya taarifa zao kusambaa kwa haraka sana kupitia waokoaji hao,” moja ya chanzo cha habari kilinukuliwa na gazeti la Daily Mail.

Asilimia kubwa na wananchi wa Thailand hawawezi kuzungumza Kiingereza hivyo kuwepo kwa kijana huyo kwenye eneo hilo kulitoa nafasi kwa waokoaji wa Uingereza kuwasiliana kwa karibu na kuanza kutoa msaada.

Mbali ya kuwa na ufasaha wa kuwasiliana kwa lugha ya Kiingereza mtoto huyo pia anauwezo wa kuzungumza lugha nyingine kama Kithai( Thailand), Burmese( lugha inayozungumzwa Mynmar) na Kichina.

Picha zao za kwanza zaibuka

Picha ya kwanza iliyopo kwenye mfumo wa video za watoto walikuwa wamekwama pangoni imetolewa zikionyesha wakiwa na kocha wao wakipatiwa matibabu katika hospitali moja.

Katika picha hiyo watoto kadhaa wanaonekana wakiwa wamefunikwa usoni isipokuwa mmoja tu anayeonyesha alama ya ushindi kupitia vidole vyake.

Operesheni ya kuwaokoa watoto hao ilikamilika Jumanne ikitumia operesheni  tatu tangu kuanza kwake ikiwahusisha waokoaji toka ndani na nje ya Thailand. Walikuwa kwenye pango hilo lilojaa maji ghafla kutokana na mvua iliyonyesha kwa muda wa siku 18.

Katika hatua nyingine, kikosi cha uaokoaji cha Thailand kimeonyesha video mpya inayoonyesha operesheni tatu za uokoaji ambazo zimevuta hisia za watu wengi duniani.

Wazamiaji wanasema watoto hao walipewa dawa ya usingizi ili kuwaondolea hofu wakati wa uokoaji na walilazwa katika kitu kama kitanda maalumu.